Ni Shein na Maalim Seif
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliwaambia wanahabari jana kuwa halmashauri kuu ya chama hicho iliyokuwa imeketi jioni ilimuidhinisha mwanasiasa huyo kuwania kiti hicho ikiwa ni awamu yake ya mwisho.
Uteuzi huo wa Dk Shein ulikuwa ni moja ya ajenda za kikao cha halmashauri hiyo ambayo pia ilikuwa na kazi nzito ya kuteua wagombea watatu wa urais wa Muungano kati ya watano waliokuwa wamepitishwa na Kamati Kuu kutoka kwenye kundi la makada 38 juzi.
Kuteuliwa kwa Dk Shein kunarudisha upinzani mkali kwa mara nyingine dhidi ya mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Wawili hao waligombea mwaka 2010 na kukabana koo katika uchaguzi visiwani humo ambao ulishuhudia Dk Shein akimwacha Seif kwa tofauti ya asilimia moja.
Matokeo hayo yalifuatiwa na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Shein akiwa Rais na Maalim Seif, Makamu wa Kwanza wa Rais baada ya kufanyika marekebisho ya Katiba mwaka huo.
Dk Shein alichukua fomu mapema wiki tatu zilizopita pasipo kuwa na mpinzani hivyo kumtengenezea njia nyeupe ya kupitishwa na CCM.
Hata hivyo, safari hii mbali na kupitishwa na CCM kuwania urais, Dk Shein atakuwa na kibarua kigumu kulinda SUK kutokana na CUF kumaliza vibaya katika Serikali hiyo baada ya mawaziri kutoka chama hicho kutoka katika Baraza la Wawakilishi na kusababisha bajeti ya SMZ ipite bila upande wa pili.
Pia, msuguano huo uliendelea zaidi pale wabunge wa CCM walipokataa Maalim Seif kutoingia ndani ya Baraza hilo kukaa eneo maalumu wakati Dk Shein anapolivunja mwezi uliopita jambo lililozua hisia tofauti juu ya mustakabali wa SUK.
SOURCE:MWANANCHI
Maoni
Chapisha Maoni