MWAKILISHI WA WFP TANZANIA ATAMBULISHA MIKAKATI MITANO YA CSP..
Shirika la chakula Duniani (WFP) limetambulisha mikakati yake mitano iliyo ndani ya Mpango Mkakati wake Mpya wa Nchi (CSP) unaotekelezwa ndani ya miaka minne kuanzia Julai 2017 hadi 2021, wenye lengo la kutokomeza njaa na utapiamlo nchini.
Akizungumza katika warsha iliyowakutanisha WFP na waandishi wa Habari za mtandaoni leo jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa WFP Tanzania, Michael Danford ameitaja mikakati hiyo kuwa, kutoa msaada wa fedha au chakula kwa wakimbizi wanaoishi katika kambi rasmi, kuondoa utapiamlo kwa kutoa huduma za lishe katika makundi yaliyo hatarini pamoja na kuwezesha uimarishwaji uwezo katika taasisi za serikali zinazojishughulisha na masuala ya lishe.
Ametaja mikakati mingine kuwa ni, kusaidia wakulima wadogo kwa kuanzisha mfumo wa thamani wa pamoja, sambamba na kuwahamasisha kutumia kilimo kinachozingatia tabia ya nchi na aina anuai za mazao.Mkakati wa mwisho ni kuifanya nchi kuwa kituo kikuu cha ubunifu.
“Wanawake na watoto wa Tanzania wameteswa sana na athari za utapiamlo huku ikiathiri 34% ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 na kwamba kudumaa kwa watoto wadogo kumeongezeka kwa kiwango cha juu. Ili kuunga mkono malengo ya serikali katika kuondoa utapiamlo, program za WFP zinalenga kumaliza utapiamlo,” amesema
Akifafanua namna ya utekelezaji wa mikakati hiyo, amesema wamepanga kutumia kiasi cha fedha dola za kimarekani milioni 455.7 kwa ajili ya kutekeleza mikakati hiyo, ambapo itanufaisha wakimbizi wapatao laki nne, wakulima 25,0000 na kunusuru watoto na watu wazima 185,000 walio hatarini kukumbwa na utapiamlo na au baa la njaa.
Amesema WFP itashirikiana na wadau mbalimbali katika utekelzaji wa mikakati hiyo, ikiwemo Shirika la Wakimbizi Duniani(UNHCR), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Mfuko wa Kusaidia Kaya Masikini nchini (TASAF).
Aidha, amesema mikakati hiyo itasaidia kutokomeza njaa nchini pamoja na kuwainua kiuchumi wakulima sambamba na kufanikisha utekelezaji wa malengo 17 ya milenia.
Source:Modewjiblog
Maoni
Chapisha Maoni