TANZANIA YAPOROMOKA VIWANGO VYA KIMATAIFA VYA UHURU WA HABARI....


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba amedai kuwa, matukio ya uvunjifu wa haki ya habari na vyombo vya habari yamesababisha Tanzania kushuka katika viwango vya kimataifa vinavyopima uhuru wa habari (World Press Freedom Index Report 2017).
Bisimba aliyasema hayo jana Julai 31, Jijini Dar es Salaam wakati akizindua ripoti ya nusu mwaka wa 2017, ya hali ya haki za binadamu nchini, ambapo alieleza kuwa Tanzania imeshuka kwa nafasi 12, kutoka nafasi ya 71 hadi 83 katika uhuru wa habari duniani.
“Nchi yetu imeendelea kupata changamoto katika haki ya kujieleza na kutoa maoni, hali hii imeshuhudiwa zaidi kutokana na utekelezaji wa sheria ya makosa ya mtandaoni, na ya Mammlaka ya Mawasiliano TCRA pamoja na nyingine zinazovunja au kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni,” alisema. 
Katika hatua nyingine, Bisimba alisema kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa ripoti hiyo, inaonyesha kuwa, haki na uhuru wa kukusanyika pamoja haki ya kuwa huru na usalama binafsi katika kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu, zimeendelea kukiukwa. 
“Katika kipindi cha nusu mwaka pia tumeshuhudia kuzuiwa kwa mikusanyiko mbalimbali ya ndani iliyofanywa na asasi za kiraia pamoja na vyama vya siasa.Katazo hili ni kinyume cha utaratibu na sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa watu kukusanyika na kutekeleza majukumu yao kisheria,” alisema.
Aliongeza kuwa “Haki ya kuwa huru na usalama binafsi imekiukwa, haki hiyo inaeleza kuwa serikali ina wajibu wa kuhakikisha kuwa haizuii uhuru wa mtu kwa kumuweka kizuini kinyume cha sheria. Kwa muda sasa tumeshuhudia matukio ya watu kukamatwa na kutiwa vizuizini bila kuambiwa makossa yao, mbaya zaidi wamekuwa wananyimwa haki yao kikatiba ya kupata dhamana ya polisi.”
“LHRC inasikitishwa na utamaduni unaoanza kujengeka ambapo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanatoa amri ya kukamatwa kwa watu mbalimbali na kukataza watu hao kupewa dhamana kinyume na sheria ya wakuu wa mikoa. Lakini tunapongeza hatua za kukemea ukiukwaji huu zilizotolewa na wziri wa Afya pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umaa wakiwataka wahusika kuzingatia sheria za nchi katika utekelezaji wa majukumu yao,”alisema.
Bisimba ameitaka Wizara ya Sheria na Katiba kuzifanyia marekebisho haraka sheria zinazobana uhuru wa kujieleza kama Sheria ya huduma za habari na sheria ya makossa ya mtandaoni.Pia amewataka watendaji wa serikali kuhakikisha kuwa hawaingilii uhuru wa kujieleza bila ya kuwa na sababu za msingi zilizoainishwa kwenye sheria.



Source:Modewjiblog




























































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..