Niyonzima atua rasmi Simba...


Klabu ya Simba kupitia afisa habari wake imethibitisha rasmi kwamba Haruna Niyonzima ni mchezaji halali wa klabu hiyo mara baada ya kumaliza mkataba na klabu yake ya zamani Yaga ambayo aliichezea msimu uliopita.
Tetesi nyingi zilizagaa kwenye vyombo mbali mbali vya habari, mitandao ya kijamii na hata kwa wadau mbali mbali wa soka kuhusu Niyonzima kusainiwa na Simba lakini klabu hiyo haikuthibitisha jambo hilo mapema.
“Haruna Niyonzima ni mchezaji halali wa Simba tumeshamalizana nae, ameshamaliza mkataba na klabu aliyokuwa anaitumikia atakuja Simba. Anaweza akaenda South Africa kuungana na kikosi au anaweza kuja moja kwa moja Dar katika safari moja na Rayon Sport na atacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports siku ya Simba Day,” ilisema taarifa ya Haji S. Manara Afisa Habari Simba SC.
Klabu ya Yanga tayari ilishatoa taarifa mapema kwamba haikufikia makubaliano na Niyonzima baada ya mchezaji huyo raia wa Rwanda kutaka dau kubwa ili aongeze mkataba mpya wa kubaki Yanga.
Niyonzima kwa sasa yupo Rwanda mapumzikoni tangu kumalizika kwa ligi kuu Tanzania bara na kwa mujibu wa Manara, Niyonzima ataungana na wachezaji wenzake wa Simba muda wowote wiki hii.



Source:Dar24




































































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..