TAASISI ZA KIFEDHA ZASHAURIWA KUWA NA MASHARTI NAFUU YA UTOAJI MIKOPO...
Taasisi mbalimbali za fedha nchini zimeshauriwa kuwa na masharti nafuu ya utoaji mikopo ili kuwarahisishia wajasiriamali kuwa na fursa rahisi ya kupata mitaji kwa minajili ya kuendeleza biashara zao.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe Godfrey Zambi amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho ya 24 ya kilimo na sherehe za Nanenane katika Viwanja vya Ngongo nje kidogo ya Manispaa ya Lindi.
Katika Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati na wananchi watapata fursa yatawasaidia wananchi kupata elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa muda mfupi lakini pia wadau kujionea na kujifunza huduma zitolewazo na serikali, mashirika ya umma na binafsi.”
Mhe Zambi alisema kuwa miongoni mwa changamoto ambazo zimekuwa mwiba mchungu kwa wajasiriamali ni pamoja na namna ya kupata mitaji kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya biashara.
Alisema mikopo kutoka benki inatolewa kwa masharti makubwa na riba kubwa jambo ambalo ni kikwazo kwa wajasiriamali ambao wana mitaji midogo lakini inarudisha nyuma ufanisi wa wao na taifa kwa ujumla wake.
Alisema kuwa Sera ya nchi inaruhusu sekta binafsi kuendesha uchumi kupitia kampuni ndogo, za kati, na wajasilimali, hivyo mitaji kwa wajasiriamali ni jambo ambalo haliepukiki.
Zambi alisema kuwa wajasiriamali wakipatiwa huduma za fedha na kukuza mitaji yao, wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Zambi amesifu maandalizi mzuri ya Sherehe hiyo inatayarishwa na kuratibiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuhusisha Taasisi, Wizara na mtu mmoja mmoja kwa wote wanaoshughulika na kilimo.
Maonesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane yanahusisha shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya umma, makampuni binafsi, mabenki, Taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Pia uzalishaji bora wa mazao ya nafaka, ubunifu wa teknolojia rahisi za kutotoa mayai, Kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, Makampuni ya mawasiliano, ambapo Taasisi za elimu zitaonyesha ubunifu wa kumsaidia mfugaji, Tiba za asili, Wasindikaji wakubwa na wadogo wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Asali, na Nta.
Source:Modewjiblog
Maoni
Chapisha Maoni