Mkutano wa maendeleo kati ya Japan na bara la Afrika wakamilika jijini Nairobi.
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe akiwa na viongozi wa Afrika wakati wa mkutano wa TICAD jijini Nairobi nchini Kenya Agosti 27, 2016.
Mkutano wa siku mbili wa Maendeleo kati ya serikali ya Japan na bara la Afrika (TICAD) umemalizika siku ya Jumapili jijini Nairobi nchini Kenya.
Huu ulikuwa ni mkutano wa sita kati ya Japan na viongozi wa Afrika, na kufanyika mara ya kwanza barani Afrika kujadili maswala ya ushirikiano wa kuinua uchumi na biashara.
Wakati wa mkutano huu, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alitangaza kuwa serikali yake itatoa Dola za Marekani Bilioni 30 kusaidia mataifa ya Afrika kujenga na kukarabati miundo mbinu, kama barabara, bandari na vituo vya kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu na afya.
Japan itatuma fedha hizo kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika, kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kufanikisha maendeleo hayo.
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe (Kushoto) akisalimiana na rais wa Chad na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wakati wa Mkutano mkuu wa maendeleo kati ya serikali ya Japan na bara la Afrika uliofanyika kati ya Agosti 27-28 jijini Nairobi nchini Kenya.
Viongozi wa Afrika wameisfia Japan kwa kuwa mshirika wa karibu wa Japan kwa kipindi kirefu sasa huku Japan ikisema hatima ya bara la Afrika ipo mikononi mwa raia wa bara hilo.
Rais Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo amesema Japan imekuwa mshirika wa karibu katika maswala ya uimarishwaji wa miundo mbinu kama bandari, barabara na nguvu za umeme.
Aidha, Kenyatta ameongeza kuwa mataifa ya Afrika hasa Kenya itaendelea kushirikiana na Mataifa kutoka bara Asia ambayo yanaonesha nia ya kulisaidia bara la Afrika kupiga hatua ya maendeleo ili kuwasaidia watu wake.
Naye rais wa Chad na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Idriss Derby amesema, msaada wa Japan kwa bara la Afrika utasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha maendeleo katika nchi mbalimbali lakini kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa.
Mbali na maswala ya biashara na uchumi, maswala ya haki za binadamu, usawa wa kijinsia hasa kwa wanawake, usalama na kupambana na ugaidi ni maswala yaliyopewa kipau mbele katika mkutano huu.
Viongozi wa Mataifa ya Afrika wakiwa na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wakati wa Mkutano mkuu wa maendeleo kati ya serikali ya Japan na bara la Afrika uliofanyika kati ya Agosti 27-28 jijini Nairobi nchini Kenya.
Japan katika hatua nyingine, imetoa hakikisho kwa viongozi wa bara la Afrika kuwa itaunga mkono jitihada za bara hilo kupata uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Huu ndio ulikuwa mkutano wa kwanza kuwahi kufanyika barani Afrika na ulihudhuriwa na zaidi ya marais 20 kutoka barani Afrika na wajumbe zaidi ya 10,000.
Uchumi na maendeleo, uimarishaji wa sekta ya afya na ushirikiano wa karibu kati ya Japan na bara la Afrika ndio maswala makubwa yaliyoafikiwa katika mkataba wa Nairobi.
Mkutano ujao wa TICAD utafanyika mwaka 2018 jijini Tokyo nchini Japan.
Source:RFI Kiswahili
Maoni
Chapisha Maoni