Aliyetumbuliwa NIDA ‘kitanzini’
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu.
DICKSON Maimu aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na wenzake saba wamepandisha kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kuhujumu uchumi.
Watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa makosa 28 ikiwemo kuhujumu uchumi na kughushi nyaraka mbalimbali na hatimaye kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. 1 Billioni.
Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Benjamini Mwakatumbula, Mhasibu Mkuu katika mamlaka hiyo, Evalin Mombori, Joseph Makani, Astery Ndege, George Ntalima , Sabina Rymond na Xavery Kayombo.
Akiwasomea mashtaka hayo, Awamu Mbagwa ambaye ni mwendesha mashtaka wa serikali, mbele ya Respeciuos Mwijage Hakimu katika mahakama hiyo amedai kuwa, watuhumiwa hao walitumia madaraka yao vibaya kipindi wakiwa watumishi wa umma.
Shitaka la kwanza ni la Kutumia madaraka vibaya ambapo mtuhumiwa Na. moja Maimu na Na. tatu Mwakatumbula walitenda makosa hayo kati ya tarehe 15 na 19 Januari 2010 Kinondoni, Dar es Salaam katika Ofisi kuu ya NIDA kwa kuilipa Sh 2.7 milioni kampuni ya Gothan International Limeted (GIL) bila kufuata taratibu za malipo ya ofisi za umma.
Shitaka la pili hadi la tatu pia yote ni ya kutumia madaraka vibaya katika ambapo watuhumiwa hao wawili wakiwa watumishi wa umma kati ya 2010, 2014, na 2016 ambapo walifanya malipo kinyume na taratibu za ofisi za umma na kusababisha hasara kwa serikali.
Shitaka la nne, ni la kuisababishia NIDA hasara ambapo mtuhumiwa namba moja (Maimu) na namba tatu (Mwakatumbula) walitenda kosa hilo kati ya tarehe 15 Januari na 6 Mei mwaka 2010 waliisababishia hasara mamlaka zaidi ya Sh 167 Millioni.
Shitaka la sita analotuhumiwa nalo mtuhumiwa wa tano pekee, (Ndege) ambaye anatuhumiwa kughushi nyaraka mbali mbali akiwa wakala wa bima (Aste) ambapo aliisababishia NIDA hasara ya Sh. 22.5 Milioni.
Johnson Jamhuri, wakili wa utetezi wa mshitakiwa Mombori na Makani ambao hawakutajwa katika mashitaka ya uhujumu uchumi alidai kuwa wateja wake, wanaweza kupewa dhamana katika mahakama hiyo kutokana na kuwa makosa yao yanadhaminika.
Wakili Mbwagwa wa serikali alidai kuwa watu hao wametajwa katika kesi inayohusishwa na uhujumu uchumi hivyo hawastahili dhamana
Hakimu Mwijage baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili amesema, atatolea uamuzi tarehe 19 Agosti, hoja zilizotolewa ili kuamua hatma ya dhamana ya washtakiwa hao wawili.
Watuhumiwa wengine watano watarudi mahakamani hapo 31 Agosti mwaka huu kwa ajili ya kesi yao kutajwa na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kuwapa dhamana watuhumiwa wa uhujumu uchumi.
Source:Mwanahalisionline.com
Maoni
Chapisha Maoni