USAJILI: Yanga, Simba yametimia
Kiungo mpya wa Yanga, Deus Kaseke akionyesha ishara ya dole, wakati akitoka kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo. Walio nyuma yake ni viongozi na Yanga na wanachama wa klabu hiyo.Picha Khatimu Naheka.
Yanga imeshinda vita ya nje ya Uwanja baada ya kuipata saini ya kiungo Deus Kaseke aliyekuwa akiwaniwa na watani wao, Simba kwa muda mrefu.
Usajili huo wa Kaseke umekamilika jana saa 6:35 mchana katika zoezi lililochukua takribani saa tatu za mazungumzo ya mwisho baada ya klabu zote mbili kukimbizana usiku kucha juzi wakimuwinda mchezaji huyo aliyemaliza mkataba na klabu yake ya Mbeya City.
Kaseke alifanikiwa kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga, hata hivyo kabla ya kusaini na mabingwa hao wa Tanzana Bara ililazimika kumuongezea malipo kufuatia Simba kuwa katika harakati za kutaka kumbadilisha mawazo.
Kaseke alitua jijini Dar es Salaam Ijumaa Mei 22, akiletwa na Yanga waliomkatia tiketi hiyo, lakini Simba ilijipanga na kutaka kumtorosha katika hoteli moja iliyopo eneo la Kariakoo kabla ya mabingwa hao kushtukia zoezi hilo na kumhamisha katika hoteli nyingine iliyopo Sinza Kumekucha jijini Dar es Salaam.
Yanga imelazimika kutumia Sh 35 milioni badala ya ile ya awali Sh 30 milioni kufuatia Simba kutoa ofa ya mwisho wakitaka kumpatia Sh 45milioni pamoja na mshahara wa Sh2milioni na gari.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha alisema klabu yake imefanikiwa kushinda vita muhimu kwa kumsajili Kaseke.
“Usajili wetu umetokana na mahitaji ya kocha wetu (Hans Pluijm), ambaye amekuwa akisisitiza anahitaji huduma ya Kaseke katika kikosi chake, kazi yetu kama uongozi ni kuhakikisha tunayafanyia kazi matakwa ya kocha na sasa tumempata Kaseke tutakuwa naye hapa kwa miaka miwili,” alisema Tiboroha.
Kaseke alisema Yanga haitajuta kumsajili na kuomba ushirikiano wa Wanayanga kwa kipindi chote atakachokuwa kwenye timu hiyo.
“Sitarajii kujutia kujiunga Yanga wala klabu kujutia kunisajili, nitajituma na kuhakikisha nakuwa miongoni mwa wachezaji watakaoipa mafanikio Yanga,” alisema Kaseke.
Mshambuliaji wa FC Platinum ya Zimbabwe, Donald Ngoma anawasili jijini leo jioni baada ya majadiliano, atasaini mkataba huo tayari kujiunga na Yanga.
Dk Tiboroha alisema kimsingi wameshakubaliana na FC Platinum kuhusiana na usajili wa mchezaji huyo mwenye kila aina ya ufundi katika kufunga mabao.
“Ujio wake ni kukamilisha yale tuliyokubaliana na uongozi wa klabu na yeye binafsi, nini kitafanyika, tusubiri matokeo ya majadiliano hayo ya mwisho,” alisema Dk Tiboroha.
Maoni
Chapisha Maoni