Uchaguzi Mkuu, CCM sasa rasmi
Mke wa Rais, Salma Kikwete akimsalimia mjumbe mwenzake wa Halmashauri Kuu ya CCM, Stephen Wasira mjini Dodoma jana. Wajumbe wengini ni Raphael Chegeni (wa pili kushoto) na Profesa Mark Mwandosya. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Dodoma. Mbio za kuwania urais na nafasi nyingine kupitia CCM zimetangazwa rasmi baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoa ratiba ikibainisha kuwa mgombea urais chama hicho tawala atajulikana Julai 12, siku mbili baada ya yule wa Zanzibar kufahamika.
“Sasa ni ‘ruksa’ kwa wanaotafuta uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama katika nafasi za urais, ubunge, udiwani na uwakilishi kuchukua fomu kwa tarehe zilizopangwa,” Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana mjini hapa. Wanaotaka kuwania urais wataanza kuchukua fomu kuanzia Juni 3 hadi Julai 2.
Nape alisema Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao ndiyo wenye jukumu la kuchagua mgombea urais wa chama hicho, utafanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11 hadi 12. Alisema mgombea urais wa Zanzibar, atapitishwa na NEC Julai 10.
Mara baada ya kupitishwa kwa ratiba ya mchakato huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Mwigulu Nchemba alijizulu wadhifa huo ili kupata fursa ya kuwania urais.
Naibu Waziri huyo wa Fedha, alimwandikia mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuomba kuachia ngazi, naye akampa nafasi kueleza nia hiyo mbele ya kikao.
Akizungumza mkutanoni hapo, Mwigulu alisema amefikia uamuzi huo kwa kuwa hawezi kuwa refa na mchezaji.
Kutokana na uamuzi huo, Rais Kikwete alimteua aliyekuwa msaidizi wake kisiasa, Rajab Luhavi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu na kuchukua nafasi ya Mwigulu.
Uchukuaji fomu urais
Akizungumzia utaratibu wa uchukuaji fomu alisema kwa wanaowania kuteuliwa kugombea urais wataanza kuchukua fomu hizo Juni 3, mwaka huu na mwisho wa kuzirejesha ni saa 10.00 jioni ya Julai 2.
Alisema muda huo wa Juni 3 hadi Julai 2, pia utatumika kwa wagombea urais kutafuta wadhamini 450 katika mikoa 15, kati ya hiyo mitatu ikiwa ya Zanzibar, kwa maana ya Pemba na Unguja.
Utaratibu wa zamani kwa wagombea uliwataka kuwa na wadhamini 250 katika mikoa 10, miwili iwe ya Zanzibar. Pemba mmoja na mwingine Unguja.
Alisema hatua hiyo ya wadhamini 450 imetokana na kuongezeka kwa idadi ya wanachama na mikoa na kwamba idadi hiyo haitakiwi kupungua wala kuzidi.(Source Mwanachi).
Maoni
Chapisha Maoni