Mh Pinda amesema serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na chama cha wanasheria wanawake nchini (TAWLA).
Waziri mkuu Mh Mizengo Pinda amesema serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na chama cha wanasheria wanawake nchini (TAWLA) kwa miaka 25 iliyofika katika kufanya uchechemuzi wa haki za wanawake na watoto na kuisaidia jamii kwa ujumla katika masuala ya kisheria ili kupata haki sawa mbele ya sheria na kuhamasisha umma kuhusu suala la uandishi wa wosia lakini amewataka kujikita kwenye kutetea haki za watu wa makundi maalum wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi, vikongwe na makabila madogomadogo maeneo ya vijijini.
Mh, Pinda ameyasema hayo baada ya kupokea maandamano ya maadhimisho ya miaka ishirini na tano ya chama hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam yaliyoanzia viwanja vya mahakama ya hakimu mkazi kisutu na kuhudhuriwa na wadau
Mbalimbali wa masuala ya sheria hapa nchini ambapo licha ya kuwasisitizia watanzania umuhimu wa kuandika wosia ili kuondoa matatizo ya mirathi pindi mwanandoa mmoja anapofariki amesema makundi hayo yamesahaulika hivyo yanahitaji msaada wa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Kwaupande wake mwenyekiti wa chama cha wanasheria wanawake Tanzania TAWLA Bi Aisha Zumo bade pamoja na kuelezea mafanikio yao kwa miaka 25 ya chama hicho ikiwemo kuwapa msaada wa kisheria wanawake wasiopungua milioni tano nchini wameiomba serikali kuunda kitengo mahususi kitakachoshughulikia mashauri ya kifamilia katika mahakama zote nia ikiwa ni kuhakikisha mashauri hayo yanashughulikiwa kwa ufanisi weledi kwa kuzingatia tamaduni zilizopo na haki za binadamu.
Maadhimisho hayo licha ya kupambwa na maandamano yaliyoongozwa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda huku wadau wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali yaliambatana na mvua iliyonyesha ghalfa katika viwanja hivyo hali iliyopelekea kukatika kwa umeme ghafla na kumlazimu waziri mkuu Mh Mizengo Pinda kusimamisha hotuba yake kwa muda na kurudi meza kuu na baada ya tatizo kushughulikiwa aliendelea na hotuba yake ambapo pia mwenyekiti wa chama hicho Bi Aisha Bade alimkabidhi waziri mkuu bango lenye ujumbe unaoshiria ushirikiano wa TAWLA na serikali katika kutetea haki za wanawake na watoto sambamba na waziri mkuu kuzindua huduma ya uandishi wa wosia mbele ya wakili kwa wananchi itakayotolewa na wanasheria wa chama hicho kote nchini.
Source(ITV)
Maoni
Chapisha Maoni