Serikali Yaeleza Sababu Za Kulifuta Gazeti La Mawio..
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (mwenye suti ya kijivu) akiwaeleza Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya Uamuzi wa Serikali wa kulifuta Gazeti la MAWIO katika Daftari la Msajili wa Magazeti mara alipokutana na waandishi hao 17 Januari 2016 katika Ukumbi wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Bw. Assah Mwambene, wa pili kulia ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia usajili wa Magazeti, Bw. Raphael Hokororo.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Serikali toka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (hayupo pichani) juu ya Uamuzi wa Serikali wa kulifuta Gazeti la MAWIO katika Daftari la Msajili wa Magazeti mara alipokutana na waandishi hao 17 Januari 2016 katika Ukumbi wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam. PICHA NA MICHUZI JR-MMG.
SERIKALI YALIFUTA GAZETI LA MAWIO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifuta kutoka katika Daftari la usajili wa magazeti, gazeti lijulikanalo kama “MAWIO”. Amri ya kulifuta Gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 55 lililotolewa tarehe 15 Januari, 2016. Uamuzi huo umetolewa kwa mjibu wa Sheria ya Magazeti Sura ya 229, kifungu 25(1).
Hatua hii pia inazuia gazeti la Mawio kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
Serikali kwa masikitiko makubwa, imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo usioridhisha wa kuandika na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi yetu.
Aidha, hatua hii ya kulifuta gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu kuanzia Juni, 2013 hadi Januari, 2016 kumtaka Mhariri wa gazeti hilo kubadili aina ya uandishi wa habari na makala katika gazeti lake, bila mafanikio.
Msajili wa magazeti kwa juhudi zake alifanya mawasiliano na mhariri wa gazeti hilo mara nane kwa lengo la kutaka afanye marekebisho ya mtindo wa kutoa habari zake lakini mhariri wa gazeti hilo hakuzingatia ushauri mzuri aliopewa na Msajili wa Magazeti.
Ninatoa wito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia sheria, Kanuni na taratibu za taaluma ya uandishi wa habari ambazo zikizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na Sheria za nchi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana navyo
Kwa upande mwingine ninatoa pongezi kwa vyombo vyote vya habari nchini vinavyozingatia maadili, weledi na Sheria zinazosimamia taaluma ya habari na sheria nyingine za nchi. Kwa namna ya pekee Serikali inawapongeza wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari ambavyo vinapofanya makosa vikielekezwa hujirekebisha na kutoa ushirikiano kwa Serikali na pia kubadili mwenendo wao; hawa ni pamoja na wahariri wa magazeti ya;
· Mwananchi Tanzania
· Mtanzania
· The East African
· Magazeti ya Daily News na Habari Leo
· Uhuru na mengineyo
Ninapenda kusisitiza kwamba Serikali inapenda kujenga uhusiano mzuri na wa kirafiki kati yake na wadau wa sekta ya habari. Aidha ninasisitiza tena wadau wa sekta hii kuzingatia Sheria ili kujenga heshima ya tasnia ya habari na kulinda amani ya nchi yetu.
Imetolewa na Nape M. Nnauye(Mb,)
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Dar es Salaam, leo tarehe 17 Januari, 2016
SOURCE:Lindi Yetu
Maoni
Chapisha Maoni