Ukawa walikomalia Jiji uchaguzi meya...
Madiwani kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa), wakiwa nje ya Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji hilo. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeunda kamati ya pamoja itakayoongozwa na mameya wa Kinondoni na Ilala kuihoji Halmashauri ya Jiji sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi wa meya wa Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeunda kamati ya pamoja itakayoongozwa na mameya wa Kinondoni na Ilala kuihoji Halmashauri ya Jiji sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi wa meya wa Dar es Salaam.
Tamko hilo lilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu kwenye viwanja vya Karimjee wakati akizungumza na wajumbe wa umoja huo waliojitokeza kwa lengo la kufanya uchaguzi wa meya wa jiji ulioahirishwa kwa taarifa fupi juzi bila ya kutoa sababu.
Alisema pia timu hiyo itahoji uhalali wa barua iliyotoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kama ina uthibitisho wa majina ya wabunge wa viti maalumu walioteuliwa na CCM kwa kuwa inaonyesha dosari kadhaa.
Kuhusu barua ya NEC, Mwalimu alisema wana shaka nayo kwa jinsi ilivyoandikwa ni tofauti na ilivyozoeleka kwa kuwa maneno yake ni makubwa na baadhi ya wabunge wa viti maalumu wamewekewa alama ya vyema, lakini ipo tofauti na waliyopewa wao.
Hata hivyo, mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima aliwaaambia wanahabari jana ofisini kwake kuwa amesikitikishwa na kauli ya Mwalimu kwani ameizungumza NEC bila kufanya utafiti.
“Labda niseme hivi ile barua ipo sahihi na mimi ndiye nimeisaini kwenda CCM, ili kuhakiki uhalali wa wabunge wao wa viti maalumu ambao walitakiwa waingie kwenye Baraza la Madiwani la Kinondoni.
“Barua zote haziwezi kufanana ingawa Chadema na wao waliomba kuhakikiwa majina na wabunge wa viti maalumu ili washiriki katika uchaguzi wa Meya wa Kinondoni,” alisema Kailima.
Alisema kazi kubwa ya NEC ni kuidhinisha majina ya wabunge wa viti maalumu yaliyopendekezwa na vyama tofauti, lakini sheria za Serikali za Mitaa ndizo zitakazowabana kuhusu makazi yao ili kuwaruhusu kuwa madiwani.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa mkoani Dar es Salaam, Bakari Shingo alisema walipokea barua kutoka ofisi ya mkurugenzi wa jiji ikiwataarifu kuwa jana uchaguzi wa meya ungefanyika, lakini walishangaa kuahirishwa ghafla.
Msemaji wa jiji, Gaston Makwembe alisema hawezi kuzungumza chochote zaidi ya kusisitiza kuwa jukumu lao lilikuwa ni kutoa taarifa kwa vyama na wananchi kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob alisema hatua ya kuahirisha uchaguzi huo haiwapi presha, bali inakwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo kwa sababu watu wa kutoa uamuzi hawapo.
Maoni
Chapisha Maoni