Wanahabari waliokamatwa Burundi waachiliwa..
Phil Moore (kushoto) alikuwa amezuiliwa pamoja na Jean Philippe Remy
Wanahabari wawili wa kigeni waliokuwa wanazuiliwa na maafisa wa polisi nchini Burundi wameachiliwa huru.
Mpiga picha Mwingereza Phil Moore na mwanahabari Mfaransa Jean Philippe Remy walikamatwa pamoja na watu wengine 15 Alhamisi jioni katika mtaa wa Nyakabiga ambao ni ngome ya upinzani mjini Bujumbura.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius alikuwa awali ameitaka Burundi kuwaachilia huru mara moja wanahabari hao.
Bw Remy hufanyia kazi gazeti la Ufaransa la Le Monde.
Ripoti kutoka Burundi zinasema wanahabari hao wameachiliwa huru baada ya kuhojiwa na maafisa wa uchunguzi wa jinai na kisha kusikizwa na mwendesha mashtaka.
Hawakufunguliwa mashtaka yoyote.
Mwandishi wa BBC aliyeko Bujumbura Prime Ndikumagenge anasema wawili hao hawajarejeshewa simu na kamera zao. Vifaa hivyo vinazuiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Baraza la kitaifa la mawasiliano nchini humo pia limefutilia mbali vibali vyao vya kuhudumu kama wanahabari nchini humo.
Maafisa wa polisi wanasema Bw Moore alikuwa pamoja na "wahalifu" hao wengine wanaozuiliwa na alikamatwa kwa sababu alitoroka pamoja nao.
Awali, chama cha wanahabari kutoka nje ya Afrika Mashariki kilisema kimesikitishwa sana na kukamatwa kwa wawili hao ambao kimesema ni "weledi katika kazi ya uanahabari”.
Wawili hao ndio wanahabari wa kwanza wa nchi za nje kukamatwa na kuziliwa Burundi tangu kuanza kwa machafuko mwezi Aprili mwaka jana.
SOURCE:BBC
Maoni
Chapisha Maoni