Chadema: Tutamalizia kwa Dk. Magufuli..
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa.
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuonya mikutano ya kisiasa ya hadhara, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeahidi kumalizia mikutano yake nyumbani kwake Chato, Geita.
Chadema Kanda ya Ziwa Victoria kimeeleza kuwa, kitahitimisha Operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) katika Wilaya ya Chato anakotokea Rais Magufuli.
Tarehe 27 Julai mwaka huu, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa alitangaza kuanza mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu chini ya mwavuli wa Ukuta.
Licha ya Chadema chini ya Mbowe kutangaza mikutano na maadamano ya amani nchi nzima, bado kumekuwepo na zuio la polisi dhidi ya vyama vya siasa nchini kufanya mikutano ya hadhara kwa kile kinachoelezwa hali ya usalama kutokuwa nzuri.
Meshack Micus, Katibu wa Chadema, Kanda ya Ziwa Victoria amesema, baada ya Mbowe kutangaza kuanza kufanyika kwa mikutano nchini, wao kama kanda wanaunga mkono tamko hilo.
Amesema, maadamano na mikutano ya hadahara yataanzia mkoani Kagera na kuishia Chato nyumbani kwa Rais Magufuli ambako amedai “huko ndio itakuwa funga kazi”.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Micus amesema, maandamano hayo yatakayoanza Wilaya ya Kyerwa (Kagera) na kumalizikia Chato mkoani Geita, lengo lake ni kumtaka Rais Magufuli kuongoza nchi kwa kufuata Katiba ya Nchi.
Meshack amesema, mikutano ya vyama vya siasa nchini ipo kisheria ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani lakini wanashangaa kuona Rais Magufuli akivunja sheria hiyo.
“Vyama vya siasa nchini haviwezi kuwaomba polisi kufanya mikutano yao, bali wajibu wao ni kuwataarifu kuhusu hilo, lakini kwa hofu ya kumuogopa Rais Magufuli, wanatumia nguvu zisizo na ziada kuzuia mikutano,” amesema Micus.
Amesema, tayari wamewapa taarifa wanachama wa chama hicho katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, hivyo kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, wataanza maandamano yatakayoanzia Kyerwa na kumalizikia Chato nyumbani kwa rais ili kumfikishia ujumbe.
Micus ameeleza kushangaa madai ya Rais Magufuli kudai wabunge wa upinzani waliondoka bungeni wakiwa wameziba midomo, huku akisahau Chadema ndiyo walioibua hoja ya ufisadi na rais kuamua kuunda Makahama ya Mafisadi.
Tungaraza Njugu, Mwenyekiti wa Operesheni Chadema Kanda Ziwa Victoria amesema, Taifa limeingiliwa na kirusi kutokana na viongozi kuacha misingi iliyokuwepo.
Njugu amesema, kiongozi mzuri anatokana na jamii iliyo bora, lakini yule asiye bora hutoka katika jamii iliyo mbovu na kwamba hali hiyo inajidhihirsha kwa Rais Magufuli anavyoendesha nchi.
Hata hivyo, Njugu amewaomba wapenda haki, waweze kuungana na Chadema kupinga unyanyasi unaofanywa kwa vyama vya siasa kuzuia mikutano na maandamano yaliyopo kisheria kwenye mujibu wa Katiba ya Nchi.
Source:Mwanahalisionline.com
Maoni
Chapisha Maoni