Rais Magufuli alichowaambia wakurugenzi wa halmashauri zote za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya..


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya hapa nchini kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi na kuondoa kero zinazowakabili kwa kujiamini, uadilifu na uaminifu.
Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 12 Julai, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam muda mfupi kabla ya wakurugenzi hao wa halmashauri kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeendeshwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutekeleza jukumu hilo la kuwaletea wananchi maendeleo na kuondoa kero zinazowakabili, wakurugenzi hao hawana budi kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo ahadi ambazo serikali ya awamu ya tano imezitoa, wakiongozwa na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 - 2020.
Aidha, amesema wakurugenzi wote wa halmashauri wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na amewataka kutosita kuchukua hatua dhidi ya watendaji ambao wamejigeuza kuwa miungu watu na wanawanyanyasa wananchi.
"Wapo watendaji wa kata ambao ni miungu watu, wanachonganisha wananchi na serikali, katumieni madaraka mliyonayo kuwaondoa kazini" Amesema Rais Magufuli
Mhe. Rais Magufuli pia amewataka wakurugenzi hao kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya serikali na ametumia nafasi hiyo kuagiza wizara zote kuanza kutumia mashine za kielektroniki (EFD) katika ukusanyaji wa mapato kwenye taasisi zote ambazo zinakusanya maduhuli.
Dkt. Magufuli amewasisitiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, ambapo kila mwezi serikali hutoa shilingi bilioni 18.777 na ametaka tabia ya wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na wafanyabiashara ama wanasiasa kujinufaisha kupitia zabuni za serikali ikome.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambao walikuwepo wamewataka wakurugenzi hao wa halmashauri kuwa watumishi bora, kusimamia vizuri rasilimali za halmashauri na kushirikiana na viongozi wa mkoa na wilaya katika halmashauri zao.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 Julai, 2016




Source:Focusmedia


















































































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..