Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu.
Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema kauli za Dk John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni za kibaguzi na zinavunja umoja wa kitaifa.
Lissu alihoji kauli ya kwamba Chadema ni marufuku kufanya siasa ilikoshinda CCM na kinyume chake ndiko ulikofikia uwezo wa Rais wetu wa kufikiri?
Aliongeza kwamba, ni hawa ndio wanaohubiri umoja wa kitaifa kila kukicha?
Lissu aliweka bayana kuwa anachoweza kujidai nacho Magufuli sio nguvu ya hoja yake bali ni nguvu ya vyombo vya mabavu anavyodhibiti.
Katika andiko hilo Lissu aliwaandishi kutoshangilia mambo ambayo yanapaswa kupuuzwa badala yake wayaweke wazi.
Kabla ya Lissu kutoa kauli hiyo, watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM jimbo la Singida Mashariki waliondoa picha kubwa ya mbunge huyo eneo la Ikungi, kwa madai ya kuelekezwa na Miraji Mtaturu, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi kwa kile kilichoelezwa kuwa picha ya Lissu haikupaswa kuwa hapo wakati Rais yupo Singida kwenye ziara yake.
Mapema leo akizungumza katika mkutano wa hadhara wilayani Manyoni, Singida Magufuli amenukuliwa akisema hajazuia maandamano wala mikutano ya siasa ila kila mtu afanye kwenye jimbo lake aliposhinda tu wala sio kwenda kwenye jimbo la mwingine.
Aidha Magufuli amesema “Wale wanaotangaza kufanya maandamano, watangulie wao wenyewe na watakiona cha mtema kuni. Mimi nataka watangulie wao wasiwatangulize watoto wa masikini,” amesema Rais Magufuli huku akiongeza kuwa;
“Wao wanakaa gesti (nyumba za kulala wageni) halafu wanawapa viroba watoto wa masikini ili watangulie kuandamana, sasa mimi nataka watangulie wao halafu waone.”
27 Julai mwaka huu, Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema taifa alitangaza kuwa chama hicho kitafanya mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima ili kupinga kile alichokiita udikteta wa serikali ya awamu ya tano.
Hayo yanajiri ikiwa ni saa chache baada ya Salumu Mwalimu Naibu Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar) kusisitiza mbele ya waandishiwa habari jijini Dar es salaam kuwa maazimio ya chama hicho yapo pale pale na kwamba maandalizi ya msingi ya utekelezaji wake yameanza.
“Hatutarudi nyuma, hatutatishika, wala hatutatetereka kufanya siasa ni wajibu wetu, siyo hisani ya mtu mmoja au kikundi cha watu. Ni wajibu wetu, ni haki yetu iliyo ndani ya sheria inayoongoza vyama vya siasa na kanuni zake,” amesema Mwalimu.
Source:Mwamahalisionline.com
Maoni
Chapisha Maoni