CCM, Ukawa wafuata kura milioni 2.8 Mbeya, Mwanza..
Dar es Salaam. Siku saba kabla ya uchaguzi, wagombea urais wa Chadema, Edward Lowassa na Dk John Magufuli (CCM) wameanza kuziwinda kura 2,846,537 katika mikoa ya Mwanza na Mbeya ili kuhakikisha zinatosha kuwaingiza Ikulu.
Wakati Dk Magufuli akianzia Dar es Salaam wenye wapigakura 2,775,295 na baadaye katika Mkoa wa Mwanza wenye wapigakura 1,448,884, Lowassa alikuwa mkoani Mbeya wenye wapigakura 1, 397,653 na alitaka kuanzia katika ngome ya chama hicho, Tunduma, lakini akakwamishwa na vipaza sauti.
Kwa nyakati tofauti wagombea hao wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo, walikuwa wakikwepa kufanya mikutano ya kampeni katika mikoa ya Mbeya na Mwanza, huku ikionekana wazi walitaka kuifanya iwe ya mwisho kimkakati kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wapigakura.
Mikoa mingine yenye wapigakura wengi ni Morogoro (1,271,951), Tabora (1,097,760), Dodoma (1,071,383), Kagera (1,051,681), Tanga (1,009,753) na Arusha (1,009,292). Mikoa hii pekee inatoa ushindi wa zaidi ya asilimia 53 ambao unatosha kumpeleka mgombea husika Ikulu.
Mikoa ya Dar es Slaam na Mwanza na Mbeya yenye wapigakura wengi imevutia macho ya vyama vyote vikubwa ambavyo licha ya kuzindulia kampeni zake, pengine vitalazimika kufungia kampeni zao katika maeneo hayo.
Magufuli Mwanza
Akiwa Mwanza, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk Magufuli aliahidi kugeuza Jiji la Mwanza kuwa Geneva ya Afrika, huku akitoa ahadi lukuki ikiwamo kujenga daraja kutoka eneo la Kigongo kwenda Busisi wilayani Sengerema.
Akihutubia umati wa watu katika viwanja vya Furahisha jana, Dk Magufuli alisema anataka kuigeuza Mwanza kuwa Geneva ya Afrika kwa kujenga daraja hilo ambalo linakadiriwa kuwa na umbali wa kilomita moja na nusu, kujenga laini ya umeme wa megawati 400 kutoka Iringa-Shinyanga hadi Mwanza.
“Licha ya kuongeza kivuko kingine, nitajenga daraja refu kutoka Kigongo hadi Busisi… watu wanaweza kuona kama ni ndoto lakini barabara za lami nilizoahidi kutoka Bukoba kwenda Mtwara kwa bajaji sasa hazipo?” alihoji Dk Magufuli.
Pia, Dk Magufuli aliahidi kupanua Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza, kuimarisha ulinzi Ziwa Victoria, kupunguza ushuru kwenye mazao ya kilimo na uvuvi na kujenga daraja la juu eneo la Furahisha.
Mgombea huyo huku akijigamba kuifahamu vizuri Mwanza kwa sababu amekulia hapo na ana makazi Mtaa wa Seleman Nassoro, alisema atahakikisha jiji hilo linakuwa kituo kikuu cha biashara kwa Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aliahidi kujenga barabara kutoka Sabasaba-Ilemela, kuhakikisha anatekeleza ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kununua meli kubwa itakayofanya safari zake kutoka Mwanza-Bukoba-Musoma, huku akidai anataka kubadilisha Mwanza kwani maendeleo yamechelewa kwa miaka mitano.
Hata hivyo, Dk Magufuli alionekana kukunwa na mapokezi makubwa aliyoyapata akisema hajawahi na kuwa yamemuongezea matumaini ya ushindi kwa asilimia 95.
“Mmekusanyika bila kujali vyama vyenu, nitakuwa rais wa wote, mimi kwangu ni kazi tu… hawa wanaotafuta urais walishapata mapokezi kama haya kweli! Hivi nipate urais niwasahau Mwanza kweli kwa maendeleo, ” alisema.
Dk Magufuli kwenye utawala wake aliahidi kumbeba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo kama mwekezaji mzawa kwani amewezesha kurusha mikutano yake ‘Live’.
Mgombea ubunge Jimbo la Ilemela kwa tiketi ya CCM, Angelina Mabula alisema yeye ni kiungo mchezeshaji na kumuahidi kuwa maendeleo yanaongezeka kwa kasi.
Mgombea wa Jimbo la Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula alimuomba Dk Magufuli kusaidia tatizo la maji, kupimwa kwa ardhi ya wananchi na kujenga barabara za katikati ya jiji kutokana na kuwa kitovu kwa nchi za Afrika Mashariki.
Jambo lililoonekana kuwavutia watu wengi ni pale Dk Magufuli alipowasili kwenye viwanja vya Furahisha, akiwa na ulinzi usiokuwa wa kawaida wa polisi waliovalia sare na askari kazu.
Pia walionekana polisi wengi wakiwamo maofisa waliofurika kila kona ya uwanja huo na wengine wakiwa wamebeba mabomu ya machozi.
Kwa hesabu ya haraka, magari za polisi aina ya Defender yaliyokuwa yameegeshwa pembeni mwa uwanja huo yalikuwa saba na magari mengine ya viongozi mbalimbali wa chama na Serikali, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo.
Watu wapoteza fahamu
Kama kile kilichotokea Jumatatu wiki hii kwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa watu kupoteza fahamu kutokana kukosa hewa kwa sababu ya umati mkubwa, jana ilitokea tena kwenye mkutano huo.
Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu (Redcross), kwa kushirikiana na wafuasi wa CCM walionekana wakihangaika huku na kule kuwasaidia kwa kutoa huduma ya kwanza.
Tingatinga uwanjani
Moja ya vitu ambavyo vilikuwa vivutio vikubwa uwanjani hapo, ni tingatinga lilipolekwa uwanjani hapo likiwa na rangi ya kijani. Hata hivyo, haikujulikana sababu ya uwapo wake ingawa wafuasi wa CCM wamekuwa wakimfananisha mgombea wao na tingatinga.
Wamtandikia Khanga
Awali, mashabiki wake walitandika khanga na vitenge katika lango la kuingia Uwanja wa Ndege Mwanza.
Mbwembwe na shamrashamra zilianza mapema asubuhi huku pikipiki zikijazana kwenye baadhi ya vituo vya kuuza mafuta, huku watu kutoka viunga mbalimbali vya Jiji la Mwanza wakitembea kwa miguu kuelekea viwanja vya Furahisha.
Pia, katikati ya mji kulikuwa kuna magari ya matangazo huku yakiwa yamejaa wafuasi wa CCM wakiimba nyimbo mbalimbali za kusifia chama hicho.
Barabara kutoka eneo la Misheni hadi uwanja wa ndege zilifungwa kuanzia saa 4:00, watu wakiwa wamepanga misururu pembeni wakiimba na wanawake wakikoleza shamrashamra kwa vigelegele.
Dk Magufuli aliwasilia Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 8:30 mchana akitokea Dar es Salaam, alipokewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo.
Msafara wake ukiongozwa na waendesha baiskeli na bodaboda ulianza safari kuelekea viwanja vya Furahisha ambako aiwasili saa 9:25 alasiri, lakini ulipofika eneo la Pasiansi ulizuiwa na wananchi na mgombea huyo kulazimika kusimama kuwasalimia na kuwaomba kura.
Kuibadili Dar es Salaam
Awali, Dk Magufuli aliahidi kulibadili jiji la Dar es Salaam kwa kujenga barabara za lami na na kutatua tatizo sugu la foleni kupitia ujenzi wa madaraja na barabara za juu maarufu kama ‘flyovers’.
Dk Magufuli aliyekuwa akifanya kampeni katika Jimbo la Segerea jana, aliwaomba wakazi wa Dar es Salaam wampatie kura ili aweze kutekeleza miradi hiyo mikubwa itakayoenda sanjari na ujenzi wa barabara mrisho zitakazopunguza foleni.
Akiwahutubia wakazi wa Vingunguti wilayani Ilala, Dk Magufuli alisema kuna baadhi ya watu watahoji alikuwa wapi kipindi cha nyuma kutekeleza miradi hiyo lakini ukweli ni kwamba Serikali zilizopita zilikuwa na kazi ya kuunganisha mikoa yote na Dar es Salaam.
“Vingunguti barabara zenu zitawekwa lami na nyingine nyingi tu ambazo zitasaidia kupunguza foleni ndiyo maana juzi mmeona tumesaini mkataba wa Sh100 bilioni kwa ajili ya kujenga flyovers pale Tazara na muda mfupi mtamwona mkandarasi kutoka Japan ataanza kujenga.
“Kwa hiyo watu wa Vingunguti mtaamua mnataka kupita juu au chini na nina uhakika watani zangu Wazaramo wataenda kupiga ngoma juu ya flyover,” alisema.
Dk Magufuli alisema atajenga makutano ya kisasa eneo la Ubungo kwa kujenga barabara za ghorofa mbili na tayari fedha za mradi huo zipo zaidi ya Sh70 bilioni chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia (WB).
Huku akishangiliwa kwa ahadi hizo, mgombea huyo alisema Serikali yake itatengeneza Daraja la Selander la kisasa lenye kilomita 7.4 litakalopita juu ya Bahari ya Hindi litakaloanzia eneo la Coco Beach hadi Hospitali ya Aga Khan.
Dk Magufuli ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ujenzi, aliahidi pia kujenga barabara kubwa ya kisasa ya njia sita kuanzia Dar es Salaam kwenda Chalinze, Pwani hadi mkoani Morogoro na kueleza kuwa tayari mkandarasi (Transaction advisor) yupo eneo la mradi na barabara hiyo itakuwa na ‘flyovers’ zaidi ya saba.
Polisi afa kwenye msafara
Wakati huo huo, askari polisi PC Yesaya mwenye namba 4946 aliyekuwa akiongoza msafara wa Dk Magufuli kutoka Mwenge kwenda Segerea amefariki dunia jana baada ya kugongana na bodaboda eneo la Ubungo mataa.
Kamanda wa polisi Wilaya ya Kinondoni, Camillius Wambura alithibitisha tukio hilo na kumtaja dereva wa bodaboda kuwa ni Shaban Idd ambaye anashikiliwa na jeshi hilo.
Ajali hiyo ilitokea saa 5:40 asubuhi na kufafanua kuwa mwili wa askari huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa wakati msafara huo ukipita eneo hilo, idd alipita ghafla na bodaboda na kugongana na askari huyo ambaye alianguka na kuumia vibaya.
Jenereta lamkwamisha Lowassa
Kwa upande wa Mbeya, Lowassa alishindwa kuhutubia baada ya jenereta iliyokuwa ikitumika kupata hitilafu na kusababisha sintofahamu kwa maelfu ya watu waliofika kwenye mkutano huo.
Kutokana na hali hiyo, mkutano huo ulioandaliwa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma, uliahirishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na sasa utafanyika leo.
Ilivyokuwa
Mapema kabla ya mkutano huo kuanza, wasanii mbalimbali wakiongozwa na Kundi la Wagosi wa Kaya walitumbuiza huku makada mbalimbali wa chama hicho wakipokezana kumwaga sera zao.
Kati yao alikuwa waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ambaye alisema kuna kila sababu ya Watanzania kufanya uamuzi ifikapo Oktoba 25.
Baada tu ya kuwasili kwa Lowassa saa 10:30 jioni uwanjani hapo, ghafla vyombo vikakata moto, hali iliyozua sintofahamu.
Ukimya ulitawala na ilipotimu saa 10:48 liliingia lori lenye spika zinazotumika kwa ajili ya matangazo ya barabarani kwani ilielezwa ni hatua mbadala wa jenereta hilo.
Hata hivyo, Mbowe alipoona muda unazidi kwenda, alipanda kwenye lori lililokuwa na jenereta hilo kuona kama kuna uwezekano wa kuliwasha tena.
Huku mafundi wakiendelea kutatua tatizo, Mbowe alishuhudia hali hiyo lakini baada ya dakika sita, ilipotimu saa 11:15 aliteremka na kwenda kujadiliana na timu yake na kuamua kuvunja mkutano.
Ilipofika saa 11:18 jioni, Mbowe alipanda jukwaani kwa kutumia kipaza sauti cha gari na kutangaza: “Mkutano wa Tunduma ni muhimu sana kwetu, kumetokea hitilafu ya vyombo vyetu vimegoma kufanya kazi.
“Sasa, tunamtoa Rais wetu na mkutano huu utafanyika kesho saa 3:00 asubuhi…,” alisema Mbowe na watu kuanza kuondoka.
Mmoja wa mafundi waliokuwa wakihangaikia jenereta hilo ambaye hakupenda jina litajwe, alisema: “Kilichotokea ‘braza’, mafuta yaliisha, sasa ilipokata moto ghafla, ikasababisha hitilafu katika mfumo mzima wa kusambaza umeme, ndiyo maana tunahangaikia, lakini kama yangeongezwa mapema, hali hii isingetokea.”
Muda wote huo gari la matangazo lilikuwa likitumbuiza, lakini kabla ya kutaka kulitumia, spika zake nazo zikakata moto ijapokuwa baada ya muda mfupi matangazo na burudani viliendelea.
Mbali na Mbowe, Lowassa alifuatana na Kingunge Ngombale Mwiru pamoja na mkewe Regina Lowassa.
Wasemavyo wafuasi
Mkazi wa Pemba, Tunduma, Jacqueline Moses alisema alikuwa na hamu ya kusikia hoja za mgombea wao lakini zikakatishwa.
Nassor Umaru alisema kuwa kwa kuwa wameambiwa kesho (leo) atakuja kusikiliza.
Mwaituka James akiwa na mtoto wake alisema: “Wameniudhi, nilitaka kumsikiliza Lowassa sasa wanatuambia kesho, wameniudhi kweli na leo niliacha kufanya biashara zangu.”
Hekaheka mitaani
Kabla ya mkutano huo, kulikuwa na hekaheka mbalimbali katika vitongoji vya mji wa Tunduma katika Mkoa wa Songwe ambako baadhi ya wafanyabiashara walifunga maduka yao wengine wakidai sababu za kiusalama wengine kutaka kumwona Lowassa.
Mfanyabiashara wa vitenge, Margreth Mwakasyege aliyekutwa akifunga mapema, alisema anahofia inaweza kutokea vurugu akapata hasara.
Wauza mitumba baadhi yao walifunga biashara zao wakidai wanataka kumsikiliza Lowassa.
“Mimi bwana nimefunga biashara yangu nataka nikasikilize mgombea urais anasema nini,” alisema mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Rashid.
Baada ya mkutano huo, mashabiki wengi wao wakiwa wa Chadema walianza kukimbia mchakamchaka huku wakiimba nyimbo mbalimbali kumsifu Lowassa.
Wakizungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huo, baadhi ya wakazi wa Tunduma walisema tatizo kubwa linalowakabili ni ukosefu wa maji.
Erica Mwansenga alisema wamekuwa wakinunua dumu la maji kwa Sh500 wakati maji ya kisima ni Sh300 na hiyo ni kwa sababu hayapatikani.
Joyce Mwamakula alisema tatizo lililopo katika jimbo hilo ni kituo cha afya cha Katete ambacho alisema kimeelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.
Neema kwa wafugaji
Akiwa Simiyu juzi, Lowassa alisema akiingia madarakani atahakikisha wafugaji katika mkoa wa Simiyu wanatengewa eneo tengefu la malisho kwa ajili ya mifugo yao.
Aliyasema hayo juzi kwa nyakati tofauti katika majimbo ya Itilima na Meatu mkoani hapa wakati akihitimisha kampeni zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“nimesikia kilio cha wafugaji na wawekezaji katika maeneo ya Hifadhi ya Pori la Akiba la Wanyamapori la Maswa, nitahakikisha ninaondoa kero hiyo kwa wafugaji kuwa na eneo tengefu kwa ajili ya malisho,” alisema Lowassa.
Mgombea huyo pia alisema kuwa atahakikisha wakulima wa zao la pamba wananufaika na kilimo hicho ambacho ndicho kinachotegemewa kuwapatia fedha wananchi wa mkoa huo kwa kilimo cha pamba kama zao kuu la uchumi.
Alisema akiingia Ikulu atahakikisha kuwa zao hilo linapata bei nzuri ili kumkomboa mkulima wa pamba na kuondokana na umaskini uliokithiri.
Imeandikwa na Midraji Ibrahim, Aidan Mhando, Ngollo John, Jesse Mikofu, Nuzulack Dausen na Fidelis Butahe
Maoni
Chapisha Maoni