CUF kuifanyia mageuzi sekta ya utalii,bandari..
Mgombea urais wa Zanzibar kwa (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad
Akizungumza na wafuasi wa chama hicho na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu jana, Maalim Seif alisema urasimu unawafanya wawekezaji kushindwa kuwekeza Zanzibar. Alisema sekta ya utalii haiwezi kuwanufaisha wananchi kama hali itaendelea kuwa kama ilivyo.
“Zanzibar inapendwa na matajiri duniani kwa ajili ya kuja kupumzika, lakini hawafiki kwa sababu hakuna hoteli zenye hadhi yao,” alisema na kuongeza:
“Matokeo yake watalii wanaofika hapa ni wale wanaolala kwenye nyumba za wageni zilizoko uswahilini na kula chakula eneo la Forodhani ambako wanatumia kiasi kidogo cha fedha kisichowanufaisha Wazanzibari.”
Alisema ili kuwavutia watalii matajiri, atakaribisha wawekezaji watakaojenga hoteli za kitalii zenye hadhi ya kimataifa.
Maalim Seif alisema tatizo la viongozi wa CCM Zanzibar wamekuwa wakiwakataa baadhi ya wawekezaji wenye uwezo kwa sababu zao binafsi.
“Fedha zipo duniani, wapo watu wa kuja kuwekeza Zanzibar, lakini wengine wanashindwa kwa sababu wanaombwa rushwa na viongozi wetu,” alisema na kuongeza kuwa atahakikisha anashawishi wawekezaji kujenga kumbi za kisasa za mikutano ya kimataifa.
Maalim Seif alisema atajenga bandari ya kisasa itakayokuwa ikitumia muda mfupi kupakia na kupakua mizigo.
“Kuna bandari katika nchi za wenzetu ambazo meli haikai bandarini kwa saa sita ila hapa kwetu inachukua wiki kwa sababu ya msongamano na vifaa duni,” alisema.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu alisema mbali na utalii na bandari, rasilimali za gesi na mafuta zitatumika kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki. “Tuna rasilimali nyingi Zanzibar tukipata viongozi wenye dira itapaa kiuchumi,” alisema.
Maoni
Chapisha Maoni