Gesi zaidi yagunduliwa pwani ya Tanzania..
Waziri wa madini na nishati wa Tanzania Sospeter Muhongo akihutubia wanahabari awali.
Tanzania imegundua takribani futi za ujazo trillioni 2.17 za Gesi katika eneo la Ruvu lililoko katika Mkoa wa Pwani kilomita chache kutoka mji mkuu wa biashara-Dar es Salaam.
Huu ni ugunduzi mkubwa zaidi wa gesi pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa Badra Masoud, Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania, ugunduzi huu wa gesi una thamani ya takribani shilingi za Tanzania trillioni 12 sawa na takribani dola za Kimarekani bilioni 6.
Tanzania bado inaamini huenda kuna gesi zaidi itagundulika kwa kuwa utafiti zaidi bado unaendelea.
Msemaji huyo wa Wizara ya Nishati amesema kuwa utafiti kuhusu Gesi hii umedumu kwa takribani miaka hamsini ukihusisha makampuni mbalimbali.
Aidha Bw Masoud amesema uvunaji wa gesi hii utaanza muda wowote mara tu baada ya kukamilika kwa miundombinu ambapo gesi nyingine itauzwa nje na nyingine itaifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akiongea na wanahabari awali alidokeza kuwa baadhi ya wakazi wa mji wa biashara wa Dar es Salaam tayari wameshaanza kunufaika moja kwa moja na gesi ambayo iligunduliwa katika maeneo mengine ya katikati ya bahari huko Mnazi Bay na Songo songo mkoani Mtwara na Lindi ambapo gharama ya matumizi ya nyumbani haivuki dola kumi za Kimarekani kwa mwezi.
Kwa mujibu wa Waziri Muhongo, Tanzania imetenga takribani dola milioni 6 za kimarekani za kufanyia tathmini na kuwalipa watu watakaokutwa katika eneo ambalo kutajengwa mtambo mkubwa wa gesi mkoani Lindi.
Mradi ambao utakuwa wa tatu kwa ukubwa katika historia ya Tanzania baada ya ule wa Reli inayoiunganisha Tanzania na Zambia, TAZARA, na bomba lililojengwa kusafirisha gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam.
Source:BBC
Maoni
Chapisha Maoni