Maafisa waandamizi wa polisi watakiwa kuwashughulikia maafisa wanaotumia beji ya polisi vibaya..
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh Charles Kitwanga amewataka viongozi wa juu wa polisi kuongeza jitihada katika kushughulikia malalamiko juu ya maafisa wanaotumia beji ya polisi vibaya kwa kuwabambikia watu kesi, kuomba na kupokea rushwa, kuchelewa kufika eneo la tukio pamoja na kuchelewesha upelelezi wa kesi.
Mh Kitwanga ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua kikao cha kazi cha maafisa waandamizi wa jeshi la polisi ambapo amewaeleza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni la kila mmoja wao lakini taarifa za kukamatwa mirungi na bangi kwa wingi ni nyingi tofauti na dawa za kulevya za viwandani.
Kwa upande wake mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Ernest Mangu amesema watatumia nguvu za kutosha kudhibiti uhalifu na kuhusu askari kuweka ulinzi bandarini wameshaanza kwa maeneo maalum na wameomba jengo ili waweze kufungua kituo cha polisi bandarini.
Baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa waliohudhuria kikao hicho wameelezea changamoto za kiutendaji wanazokabiliana nazo ikiwemo tatizo la wimbi la wahamiaji haramu hasa katika mikoa ya mipakani.
SOURCE:ITV
Maoni
Chapisha Maoni