Tabia 7 Zitakazo Kufanya Uendelee Kuwa Maskini, Hata Kama Una kipato Kikubwa..


Matumaini yangu umeianza siku ya leo ukiwa na afya tele na pia una hamasa kubwa ya kujifunza kama ilivyokawaida. Nami bila choyo yoyote nakukaribisha katika darasa kuweza kujifunza.

Leo katika makala yetu ya leo naomba nianze kwa kukuuliza swali, hivi umeshawahi kujiuliza ni kwa nini kuna wakati unaweza ukawa una pesa lakini unashangaa hizo pesa kwa kipindi kifupi tu hauna tena na huelewi  hata zimeishaje au zimetumikaje?

Tena inawezekana pesa hizo ukawa umezipata za mshahara au za biashara ya aina fulani lakini kitu cha kushangaza kwa muda mfupi hizo pesa huna tena hakuna cha maana ulichonunua. Ni kitu ambacho mara nyingi kinawashangaza wengi na kushindwa kuelewa hizo pesa zimetumikaje hadi kuisha.

Naamini pia ni jambo ambalo limewahi kukutokea kwa namna moja au nyingine na kukuacha ukiwa kwenye maswali mengi sana bila kupata majibu. Lakini kama hukujua sababu hiyo isiwe tabu sana kwako.  Hali hiyo mara nyingi inasababishwa kwako na kitu kimoja tu ambacho ni tabia zako tu, hakuna kingine.

Kwa tabia hizohizo ulizonazo  kuna wakati huwa zinakuongoza kutumia pesa kwa mtindo fulani hivi ambao unakufanya uishiwe bila hata kujielewa. Unashangaa, ndiyo huo ndo ukweli wenyewe. Pia ni tabia hizohizo ikiwa utaziendekeza hata uwe na kipato kikubwa vipi ni lazima utaendelea kubaki maskini.

Najua una hamu ya kujua hili linatokea vipi? Inakuwaje tabia nilizonazo zinaweza kunifanya nikaishia kuwa maskini hata kama naingiza au nina kipato kikubwa? Ni rahisi tu kubaki kwenye umaskini ukiwa utaendekeza tabia hizi ambazo tunakwenda kuzijadili hapa.  Sasa twende pamoja kwenye makala hii kujifunza.

1. Kuwa na matumizi makubwa Ya Pesa.
Huwezi kukwepa kuishiwa, ikiwa matumizi yako kila mara ni makubwa. Inapotokea kila wakati ukajikuta una matumizi makubwa ya pesa usishangae pesa zako zikaisha kama upepo. Hapa ndipo wengi hujikuta kama wakijiloga wao wenyewe na kuanza kujilaumu.

Katika hali ya kawaida haiwezekani leo hii umepata pesa halafu maeneo kama baa ikawa ndio rafiki yako kila siku, halafu ukategemea ubaki na pesa haiwezekani. Kama una matumizi mabovu usitegemee mabadiliko makubwa yoyote zaidi utabaki kwenye umaskini. Kuwa makini sana na matumizi yako, vinginevyo utabaki kuwa maskini.

2. Kushindwa kuwekeza maeneo mengi.
Kosa kubwa linalofanywa na watu wengi ni kuendelea kuwekeza eneo moja wakati wanakipato kikubwa. Kwa kifupi, wanakuwa ni watu wa kuisahau kesho yao kwa kushindwa kuwekeza tena na tena maeneo mengine na kushikilia sehemu moja walipo.

Ili uweze kuwa na mafanikio ni lazima ujifunze kuwekeza zaidi na pesa uliyonayo. Ifanye pesa yako ikuzalishie zaidi ya hapo na acha kuitumia yote. Kushindwa kufanya hivyo itakupelekea kutabaki kuwa maskini ingawa kipato chako ni kikubwa.

3. Kutokujiwekea Akiba.
Kwa kawaida unapokuwa na pesa tena ukiwa kijana ni rahisi sana kutumia pesa zako hovyo kwa mambo yasiyo ya lazima kama starehe na kusahau kujiwekea akiba. Na pia inaweza ikawa rahisi kwako kuwaza muda wa kuwekeza bado na ukaendelea kusubiri.

Kitu usichokijua hapo unakuwa unapoteza muda kwa kuendelea kusubiri. Kwa kiasi chochote cha pesa ulichonacho ni vizuri ukaanza kujiwekea akiba moja kwa moja. Acha kutumia ndo uweke akiba, weka kwanza akiba yako na pesa iliyobaki itumie. Ukijisahau katika hili rafiki, utabaki kwenye umaskini.

4. Kutokuweka kumbukumbu ya matumizi ya pesa zako.
Kuna wakati wengi wetu huwa tunafikiri tunajua sana hasa kule pesa zetu zinakotoka na zinapokwenda. Kwa mazingira haya husababisha kuacha kujiwekea kumbukumbu kabisa ya pesa zetu. Lakini kwa huzuni, ni kwamba wengi wetu huwa hatujui tunatumiaje pesa hizo na kujikuta zimeisha.

Yale mambo madogo madogo tunayoyadharau kama ofa ndogo ndogo, simu zisizo na maana yanatupotezea pesa nyingi sana. Njia bora itakayokusaidia kulinda kipato chako na kuondokana na janga la kuendelea kuwa maskini huku unakipato kikubwa ni kujiwekea kumbukumbu ya pesa zako zote. Chochote unachotumia weka kumbukumbu yake.

5. Kukosa Bajeti.
Unaweza ukawa unajiwekea kumbukumbu vizuri kwa kila pesa unayoipata, lakini kama unajisahau kujiwekea bajeti basi itakuwa ni kazi bure. Kuwa na bajeti inayokuongoza ni msingi mkubwa wa ulinzi wa pesa zako zinazopotea hovyo na mafanikio kwa ujumla.

Kitu cha kufanya unatakiwa kuweka bajeti yako na kuifata. Bajeti hiyo ambayo utakayoiweka itakufanya uwe makini sana na kila matumizi ya pesa yanayokuja mbele yako. Lakini endapo unakuwa unaishi kiholela bila ya bajeti, basi hata kama unakipato kikubwa ni rahisi kuendelea kuwa maskini.

6. Kutokuwa makini na mahitaji ya lazima.
Kama lengo lako kubwa ni kuweka akiba na kujenga utajiri, ni lazima sasa uwe makini na vile vitu unavyovifanya kwa matumizi ya lazima unapokuwa na pesa. Inatakiwa ujue jambo lipi la lazima kwangu kulifanya nikiwa na pesa na ni jambo lipi lisilo la lazima.

Wengi wanashindwa kufikia lengo la kuwa huru kifedha kutokana na kupoteza umakini kwa mambo ya lazima. Kwa kifupi naweza nikasema wanajichanganya wao wenyewe. Kwa lugha rahisi unatakiwa kuwa makini na matumizi yako ya lazima ili kufanikiwa. Lakini ukitumia tu eti kwa sababu una kipato kikubwa utapotea.

7. Kusahau madeni yako.
Jjifunze kutokujilimbikizia madeni mengi ili kufanikiwa. Kama kuna deni la pango, karo za watoto na mengineyo mengi yalipe mapema sana. Lakini kujilimbikizia madeni mengi hata kama unakipato kikubwa vipi hiyo itakuwa ni mzigo mkubwa kwako na utabaki kuwa maskini.

Kaa chini na tafakari yale meneo yote unayodaiwa na yanayokusumbua. Ukishayagundua yafanyiwe marekebisho. Ukishalipa madeni yako anza sasa kujijengea utajiri kwa kuwekeza kwa kadri unavyotaka wewe. Kikubwa acha kusahau kulipa madeni yako mapema, usipofanya hivyo utarudishwa nyuma sana kimafanikio.

Chukua hatua juu ya maisha yako. Jijengee tabia za kimafanikio wakati unapokuwa na pesa ili zikusaidie kukujengea utajiri na si kukurudisha nyuma. Kwa kifupi hizo ndizo tabia zenye uwezo wa kukufanya ukabaki kuwa maskini hata kama una kipato kikubwa.




Source:Muungwana Blog

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..