Maafisa wa TAKUKURU watakiwa kuorodhesha tena mali zao..
Waziri katika Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki
Rungu la uwajibishwaji watumishi wa umma wa Tanzania limeingia kwa wafanyakazi na Maafisa wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Tanzania- TAKUKURU ambao wametakiwa kuorodhesha upya mali zao baada ya kubainika taarifa za awali za baadhi ya watumishi hao kutokuwa za kweli.
Agizo hilo limetolewa Jumatatu na waziri wa nchi ofisi ya rais anaesimamia Utumishi na Utawala Bora Angela Kairuki ambaye alidai kubaini kuwepo kwa taarifa za uwongo juu ya mali halisi zinazomilikiwa na baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini humo.
Waziri Kairuki alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtumishi yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo hilo la kudanganya umiliki wa mali zao.
Aidha katika kupambana na vitendo vya rushwa ndani ya taasisi hiyo ya TAKUKURU aliagiza kufanyika uchunguzi kwa maafisa wote wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kutomaliza upelelezi kwa wakati unaotakiwa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, Ummy Mwalimu
Wakati huo huo jijini Dar Es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alimuagiza mwenyekiti wa Bodi ya Bohari ya Dawa Tanzania-MSD kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne wa bohari hiyo kwa madai ya kukiuka taratibu za manunuzi ya dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilion 1.5 katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2015.
Waziri Ummy alisema kuwa wakurugenzi hao wanne wanasimamishwa kupisha uchunguzi baada ya ripoti ya ukaguzi ya Deloitte na Global Fund kubainisha kuwepo na manunuzi yenye kutia shaka, hatua iliyotishia nchi wafadhili kususia kuchangia fedha za manunuzi ya dawa iwapo hakuna hatua zitakazochukuliwa na serikali.
SOURCE:VOA
Maoni
Chapisha Maoni