Necta yazuia matokeo ya wanafunzi 55..
Wazazi hao waliandamana jana kwa lengo la kutaka maelezo baada ya uongozi wa shule hiyo ya Kihanga kutowapa ufafanuzi, kwa kuwa ada ya mitihani walilipa, hivyo wanashangaa kuambiwa matokeo yamezuiliwa.
Mzazi, Arcard Kanani alisema wao kama wazazi walitimiza malipo yote ikiwamo michango mingine, kama walivyotakiwa.
“Tumelipa ada, mimi nililipa Februari 24, 2015 na stakabadhi ninazo, lakini naambiwa sikulipia, hili ni jipu linatakiwa kutumbuliwa leo,” alisema Kanani.
Paulina Nkuba alisema alijinyima kuhakikisha analipa kila mahitaji ya mtoto wake, lakini anashangazwa kuzuiwa kwa matokeo.
Mwanafunzi Happiness Salvatory, alisema gharama zote za shule alifadhiriwa na Shirika la Tumaini Fund, maelezo yaliyothibishwa na Mkamu Mkuu wa Sekondari, James Bilusya kuwa fedha hizo zililipwa.
Wazazi hao walidai fedha zao zilipokewa na aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Martin Jiyu ambaye kwa sasa amehamishiwa shule ya Sekondari Kiruruma.
Hata hivyo, Mwalimu Jiyu alisema malipo hayo yalikuwa yanakusanywa na watu watatu, hivyo alizopokea na kuzituma matokeo yao yametolewa na Necta.
“Ni kweli matokeo yamezuiwa lakini niliacha mambo yote yapo sawa na nimeshahamishwa kituo cha kazi, ila nipo njiani naelekea ofisi ya ofisa elimu nimeitwa haraka ili kutoa ufafanuzi zaidi,” alisema Mwalimu Jiyu.
Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Karagwe, Kedesi Ruselu alisema kilichofanyika ni kosa tena la jinai, hivyo aliwaomba wazazi hao kuwa wavumilivu kwa sababu suala hilo wanalifanyia kazi ndani ya muda mfupi watapatiwa suluhisho.
Maoni
Chapisha Maoni