Serikali yasifu maandamano ya utulivu...

“Tunaomba wanasiasa na mashabiki wao wasitembee
“Tunaomba wanasiasa na mashabiki wao wasitembee na silaha kwenye mikutano yao, waziache mahali salama nyumbani na pia wawaache polisi wafanye kazi yao ya kuwalinda wote.” Chikawe 

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe amesema wamefurahishwa na amani iliyotawala wakati wa maandamano ya kumsindikiza mgombea wa urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Edward Lowassa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu juzi.
Waziri Chikawe alisema jana kuwa alishuhudia umati mkubwa wa watu wakiimba na kucheza katika hali ya amani na hilo ni jambo zuri linalopasa kuendelea wakati wote.
Alisema anatarajia hali hiyo itaendelea hata mikoani mgombea huyo akienda.
“Tumefurahi, kulikuwa na amani ya kutosha, watu walikuwa wengi zaidi ya ilivyokuwa kwa CCM,” alisema Waziri Chikawe.
Waziri Chikawe alikiri maandamano hayo kusimamisha shughuli katika baadhi ya maeneo ikiwamo ofisi yake ambayo haikupokea wageni kwa saa kadhaa.
Wakati huohuo, Chikawe alionya: “Tunaomba wanasiasa na mashabiki wao wasitembee na silaha kwenye mikutano yao, waziache mahali salama nyumbani na pia wawaache polisi wafanye kazi yao ya kuwalinda wote.”
Waziri Chikawe alisema mabomu ya machozi yanayotumika kazi yake siyo kuua au kuumiza watu bali kuzuia wasifanye vurugu.
Hata hivyo, Waziri Chikawe alisisistiza ushiriki wa viongozi wa vyama vya siasa ni muhimu katika kufanikisha hilo.
Alisema wanasiasa wanapaswa kujiheshimu kwa kukwepa kampeni za uchochezi na kauli zinazoweza kusababisha fujo.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwaambia Watanzania kwamba tutakuwa na uchaguzi wa amani na utulivu, hiyo ndiyo dhamira yetu, lakini hilo linaweza kufanikiwa iwapo tutapata ushirikiano kutoka kwa vyama vya siasa na mashabiki wao,” alisema Waziri Chikawe.
Alisema Serikali imejipanga kuhakikishia Watanzania wanaendelea kuwa na amani.
“Tutahakikisha watu wanapiga kura kwa amani, sina wasiwasi na eneo hilo. Naomba viongozi wa siasa watusaidie, tusingependa kufikia hatua ya kupiga mabomu wakati wote...tunataka  tumalize mchakato huu kwa amani,” alisema.
Alisema dhamana ya damu ya Watanzania katika kipindi hiki iko mikononi mwake na asingependa kuona yeyote anapata maradha.
“Viongozi wa vyama wana nafasi kubwa katika kutekeleza hilo, tunaomba wasilete vurugu, wasitishane na pia wasitumie silaha wala kufanya fujo,” alisema  Waziri Chikawe.

SOURCE:Mwananchi








Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..