Wenyeviti watatu CCM waachia ngazi..
Bukoba/Sumbawanga. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Manispaa ya Bukoba, Chifu Karumuna amebwaga manyanga na kujiunga na Chadema.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi mpya ya Chadema juzi, mwenyekiti huyo wa zamani wa UVCCM, ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Kahororo alisema hakutendewa haki na chama chake, alichokituhumu kumpora ushindi pamoja na kuongoza katika kura za maoni kutetea wadhifa wake.
Jina la Karumuna liliondolewa kwa madai kuwa hakuwa na sifa za kugombea udiwani, uamuzi alioupinga na kuamua kuhamia Chadema.
Karumuna anadaiwa kuondoka na wanachama wengine zaidi ya 100 kutoka CCM.
Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Bukoba, Victor Sherejei alisema Karumuna amechukua uamuzi wa busara, kwani hata kabla ya kuhama CCM alikuwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Emmanuel Kilindu na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wilaya hiyo, Michael Chifunda wametangaza kujiuzulu nyadhifa zao.
Kilindu alisema wameamua kujiuzulu nafasi hizo kwa kuhofia usalama wa maisha yao na familia zao.
Alisema kujiuzulu kwao kunatokana na kuvuja kwa siri za ndani za mchakato wa kura za maoni, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
Mwenyekiti huyo alimtuhumu mmoja wa wagombea kwenye kura za maoni kutuma kundi la vijana kwa ajili kumdhuru, huku pia akitishiwa kuchomewa moto nyumba yake na ofisi ya CCM. Alisema pamoja na kwamba hakutoa taarifa za vitisho hivyo polisi, lakini uamuzi wa kujiuzulu ndiyo njia pekee ya kuokoa maisha yake.
SOURCE:Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni