Ivo afanyiwa zengwe Simba...
TIMU ya Simba imemtema kipa wake Ivo Mapunda, huku ikielezwa kuwa mkongwe huyo ameondoka katika timu hiyo baada ya kusukiwa zengwe ndani ya miamba hiyo.
Ivo alitua Simba Desemba mwaka juzi akitokea Gor Mahia ya Kenya, likiwa ni pendekezo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mcroatia Zdravko Logarusic na kusaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu uliomalizika Mei mwaka huu.
Baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Yanga, ambapo Wekundu hao walishinda bao 1-0, Ivo aling’ara na kumkuna Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Poppe, aliyedai watampa mkataba wa mwaka mmoja.
Lakini hali imekuwa tofauti baada ya uongozi wa Simba kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Haji Manara, kutangaza kuachana na kipa huyo kwa kile walichodai amedengua kusaini mkataba mpya waliompa.
“Tumeachana rasmi ya kipa wetu Ivo Mapunda, tulimpa mkataba mpyalakini alishindwa kusaini ndani ya muda tuliowekeana hivyo hatutakuwa naye tena msimu ujao,” alisema.
Hata hivyo, habari za kuaminika zilizolifikia MTANZANIA zimedai kuwa kulikuwa na mgongano mkubwa baina ya viongozi wa Simba juu ya kuongezewa mkataba kwa kipa huyo. Taarifa hizo zimedai kuwa kikao kilichoketi hivi
karibuni kupitia mambo mbalimbali ya timu hiyo, kilifikia uamuzi huo wa kutompa mkataba wa mwaka mmoja.
“Wajumbe wengi walishindwa kuukubali uwezo wa Ivo Mapunda, baada ya kudai hana mapenzi na timu hiyo na alifungwa baadhi ya mabao mepes sana, ikiwemo mchezo muhimu waliofungwa na Mbeya City mabao 2-0 mkoani Mbeya, mechi ambayo ilikuwa muhimu sana na tulitakiwa kushinda ili kuendelea kuifukuza Azam,” alisema.
Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Ivo Mapunda kuzungumzia suala hilo, ambaye alikanusha taarifa za yeye
kukataa kusaini mkataba na kudai alikuwa hatakiwi ndani ya Simba.
“Taarifa za mimi kutemwa nimezisikia kwenye vyombo vya habari, ila si kweli kuwa mimi nimekataa kusaini mkataba mpya.
Kama ndio hivyo kwanini mimi nilienda kwenye kambi ya Lushoto hadi nikaumia ndio nikaondolewa kambini kwa
matibabu, ila ukweli mimi nilikuwa sitakiwi Simba,” alisema.
Alieleza kwa sasa yupo huru kujiunga na timu yoyote hapa nchini, itakayokuwa na ofa nzuri huku akiwa na mipango mingine ya kucheza soka la kulipwa.
Kocha wa Simba, Dylan Kerr, akishirikiana na Kocha wa Makipa, Abdul Salim, wameshaanza kusaka kipa mzoefu wa kuziba nafasi yake ikiwa inamjaribu Muivory Coast, Vincent Angban na Mreno Ricardo Andrade, anayetarajia kutua muda wowote kuanzia sasa.
SOURCE:Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni