Lipumba arejea, aapa kutounga mkono Ukawa...
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Rwanda jana.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alirejea nchini jana jioni akitokea Kigali, Rwanda alikokwenda mara tu baada ya kujiuzulu wadhifa huo siku nane zilizopita.
Profesa Lipumba aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) saa 10.10 jioni kwa ndege ya Rwanda Air.
Akihojiwa na Azam Tv kwa simu akiwa Kigali, siku tatu baada ya kuondoka nchini, Profesa Lipumba alisema alikuwa nchini humo akifanya utafiti kuona namna gani Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.
Alipoulizwa jana, Profesa Lipumba alisema akiwa huko alikuwa na mazungumzo na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), wadau wa masuala ya rushwa, waziri wa fedha wa nchi hiyo na makamu mwenyekiti wa Bodi ya Utawala.
“Wenzetu wamepiga hatua kubwa katika kukuza uchumi ndani ya kipindi kifupi, hivyo safari yangu ilikuwa ya kujifunza mbinu walizotumia kufikia malengo yao,” alisema.
Akizungumzia hatima yake kisiasa, licha ya kusema ataendelea kuwa mwanachama wa CUF, alisema hatashiriki kufanya kampeni kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuwa umoja huo umemsimamisha mwanachana wa CCM, Edward Lowassa.
“Kisiasa hatima yangu ni kama ya Mtanzania mwingine yeyote, Ukawa tuna mgombea kutoka CCM, amehama juzi tu, pia mle ndani ya Bunge la Katiba hakuunga mkongo Rasimu ya Katiba na ndiyo maana nikasema dhamira yangu inanisuta,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema wanachama wa CUF hawana sababu ya kuona kama amewaacha kwa kuwa bado yupo nchini.
Awali, akitangaza kujiuzulu, nguli huyo wa uchumi, alisema alifikia uamuzi huo kutokana na Ukawa kumkaribisha Lowassa kugombea urais kupitia umoja huo, hivyo dhamira yake inamsuta.
SOURCE:Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni