Lowassa kwenda NEC kupitia CUF...
Naibu Katibu mkuu wa Chadema Taifa upande wa Zanzibar Salum Mwalimu akizungumza wakati wa mkutano na waandishi Dar es Salaam jana. Katikati ni Katibu Mkuu wa NDL Tozzy Matwanga na kulia ni Rajabu Kazimoto wa NCCR-Mageuzi. Picha na Salim Shao.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kesho atachukua fomu za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati msafara wake utakapoanzia ofisi za makao makuu ya CUF kuelekea ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na baadaye kwenda kumalizia makao makuu ya Chadema yaliyoko Kinondoni.
Safari ya Lowassa, ambaye anawania urais kwa tiketi ya Chadema na chini ya mwamvuli wa vyama vinne vya CUF, NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, itakuwa ya umbali wa kilomita 11, ikihusisha wilaya mbili za Ilala na Kinondoni.
“Yeyote anayejisikia kutaka kumsindikiza Lowassa, anakaribishwa,” alisema kaimu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu jana alipozungumza na waandishi wa habari.
“Tutaanzia CUF na kumalizia Chadema. (Lowassa) ataambatana na mgombea mwenza, Juma Duni Haji.”
Kwa mujibu wa Mwalimu, msafara huo utaanzia ofisi hizo za CUF zilizoko Buguruni na kwenda katikati ya jiji, takriban kilomita tano, ambako Lowassa atachukua fomu ofisi hizo za NEC na baada ya tukio hilo, msafara utakwenda Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, takriban kilomita sita, ambako ni makao makuu ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Lowassa, ambaye alibadili upepo wa mbio za urais baada ya kuihama CCM na kujiunga na Chadema iliyompa fursa ya kuwania nafasi hiyo, atakuwa mtu wa saba kuchukua fomu hizo tayari kwa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25. Wengine waliochukua fomu hizo ni John Magufuli wa CCM, Mchungaji Christopher Mtikila (DP), Chifu Lutayosa Chemba (ADC), Macmillan Limo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma), Fahami Dovutwa (UPDP) na Dk Godfrey Malisa (CCK).
Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya NCCR jana, Mwalimu alisema msafara wa kumsindikiza Lowassa utaanzia saa 3:00 asubuhi.
Alisema mara baada ya kukamilisha kazi ya uchukuaji fomu, kuanzia Agosti 14, Lowassa ataanza ziara katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutafuta wadhamini, ikiwa ni baada ya kushiriki mazishi ya kada mkongwe wa CCM, Peter Kisumo yatakayofanyika Agosti 13, mkoani Kilimanjaro.
“Hatakwenda mikoa yote kutokana na muda, lakini tatizo jingine kila mwanachama anataka mgombea wetu (Lowassa) aende mkoa aliopo. Hili limetupa tabu na ndiyo sababu ya kubadilika kwa ratiba zetu,” alisema.
“Tutaeleza ratiba kamili na katika mikoa ambayo Lowassa hatafika kwa sasa, atafika wakati wa kampeni,” alisema Mwalimu.
Kuhusu ugawaji wa majimbo, Mwalimu alisema kazi hiyo imeshafanyika na siku yoyote kuanzia leo watatangaza.
“Tumeyagawa majimbo yote yakiwemo yale 26 mapya kwa kuzingatia umoja wetu wa Ukawa. Najua siku zimebaki chache kabla ya uchaguzi mkuu, hivyo tutatangaza tu kuanzia kesho (leo),” alisema.
Katika hatua nyingine, Mwalimu aliitahadharisha CCM na NEC akizitaka ziache kile alichokiita “mchezo mchafu” wa kufanya uchakachuaji wa kadi za kupigiakura.
“Kuna maelekezo nchi nzima ya vyombo vya dola kuwataka maofisa na watumishi wa vyombo hivyo kuwasilisha kadi zao za kupigia kura na maeneo mengine namba za wapigakura zikinukuliwa. Tunaitaka NEC na CCM watambue kuwa wimbi la mageuzi haliwezi kuzuiwa kwa namna yoyote,” alidai.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey alikwisha toa onya kwamba mtu yoyote haruhusiwi kutoa kadi yake ya kupigakura au taarifa za kadi hiyo kwa ndugu, jamaa au mwajiri wake.
“Alipoulizwa kitendo cha Profesa Ibrahim Lipumba kujivua uenyekiti wa CUF, Mwalimu alisema uamuzi huo haujaitikisa Ukawa na inaendelea na mchakato wa kuchukua nchi.
“Kitendo chake cha kujivua uenyekiti wakati ambao Ukawa tunataka kwenda Ikulu, kinaonyesha kuwa hakupenda sisi tusonge mbele. Tutaendeleza harakati zetu bila yeye na kwa umoja ule ule,” alisema.
Maoni
Chapisha Maoni