Chelsea waanza vibaya...
Chelsea wameanza Ligi Kuu ya England (EPL) kwa sare na pia kipa wao namba moja, Thibaut Courtois kupewa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya.
Walikwenda sare ya 2-2 dhidi ya Swansea wakicheza Stamford Bridge, na kama Manchester United, bao moja la Chelsea lilikuwa la ‘zawadi’ kutoka kwa Federico Fernandez.
Bao jingine la Chelsea lilifungwa na Oscar ambaye baadaye ilibidi atoke nje kumpisha kipa namba mbili, Asmir Begovic kuziba pengo la Courtois.
Swansea walifunga kupitia mchezaji wao mpya, Andre Ayew wa Ghana na Bafetimbi Gomis aliyetia kimiani penati baada ya kuangushwa na kipa Courtois dakika ya 52.
Chelsea walionekana kuchoka na hawakucheza vyema kipindi cha pili, na kocha Jose Mourinho aliwalaumu watu wa benchi lake la utabibu kwa kumchukua na kumganga Eden Hazard nje ya uwanja wakiwa tayari pungufu, huku akiamini Mbelgiji huyo hakuhitaji matibabu.
Hazard alikuwa amegongana na mchezaji wa Swansea na Mourinho alitaka aendelee tu kucheza.
Alitumia mshambuliaji anayemwamini, Diego Costa na dakika za mwisho alimwingiza aliyemchukua kwa mkopo Monaco, na Radamel Falcao ambaye hakufurukuta Manchester United msimu uliopita.
Mourinho aliyeongeza mkataba wa miaka minne Ijumaa hii, ameonya kwamba kutosajili wachezaji wapya wa kiwango cha juu kunaweka timu mahali pabaya katika kutetea ubingwa wao.
Leicester.
Katika mechi nyingine, kocha mpya wa Leicester City, Mtaliano Claudio Ranieri alianza kazi yake vyema kwa kuwatandika Sunderland 4-2.
Timu iliyoingia EPL kwa mara ya kwanza msimu huu, Bournemouth walianza vibaya kwa kulala 0-1 nyumbani kwao walipocheza na Aston Villa.
Everton wakicheza nyumbani Goodison Park walitoshana nguvu 2-2 na wageni wengine, Watford.
Norwich waliopanda pia msimu huu walianza vibaya zaidi ya wengine wote kwa kufungwa 3-1 na Crystal Palace.
Kwenye mechi ya kwanza kabisa ya EPL msimu huu, Manchester United wakionekana pia kutojipanga vyema walishinda 1-0 dhidi ya Tottenham Hotspur.
Kwenye mechi hiyo, kipa namba moja, David De Gea alikuwa jukwaani akitazama mpira huo, baada ya kocha Louis van Gaal akisema si mchezaji yule yule wa msimu uliopita na asingemudu pambano hilo.
SOURCE:Tanzania sports
Maoni
Chapisha Maoni