CCM yahaha kuwaokoa mawaziri waliobwagwa...
KATIKA kile kinachoweza kutafsiriwa kama njia ya kuwaokoa mawaziri waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kamati Kuu (CC) imefuta matokeo ya awali na kutangazwa kufanyika upya kwa uchaguzi upya kwenye majimbo matano.
Kutokana na kufutwa kwa matokeo hayo, CC imeamuru kurudiwa kwa kura za maoni kesho, na matokeo yake kuwasilishwa haraka ngazi za juu kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema uamuzi huo umefanyika kutokana na kubainika dosari mbalimbali wakati wa upigaji kura za maoni uliopita.
Alisema marudio ya uchaguzi wa kura za maoni yatafanyika katika majimbo ya Kilolo (Iringa), Rufiji (Pwani) ambalo lipo chini ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Makete (Njombe) analowania Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Busega (Simiyu) lililo chini ya Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani na Ukonga (Dar es Salaam).
“Upigaji wa kura utafanyika siku ya Alhamisi Julai 13, mwaka huu (kesho) na kisha matokeo yaletwe haraka kwenye vikao vya maamuzi kwa ajili ya kufanya uamuzi wa mwisho,’’ alisema Nape.
Alipoulizwa dosari zilizobainika, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa ndani, huku akitaka utekelezwaji wa maagizo hayo kwa mujibu wa utaratibu.
UTATA ULIVYOANZA
Kurudia kwa kura za maoni kunatokana na utata ulioibuka ambapo katika Jimbo la Busega uliibuka mvutano mkali uliosababisha matokeo kutangazwa baada ya siku tatu.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, Msimamizi wa Uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Busega, William Bendeke, alimtangaza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Dk. Raphael Chegeni kuwa mshindi kwa kumbwaga Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani.
Akitangaza matokeo ya kura hizo za maoni zilizozua utata miongoni mwa wana CCM, ikiwamo kuibuka kwa tuhuma za rushwa na hata kadi hewa za chama, Bendeke, alisema Dk. Chegeni alipata kura 13,048 dhidi ya 11,829 alizopata Dk. Kamani.
Katika Jimbo la Kilolo, licha ya Mbunge anayemaliza muda wake, Profesa Peter Msola kupinga matokeo na hata kurudiwa kwa uchaguzi katika kata tatu, bado uchaguzi huo umeonekana haukuwa huru na wa haki.
Pamoja na kujitokeza dosari katika kura za maoni na kurudiwa kwa uchaguzi, wana CCM wa maeneo husika walisusia, hali iliyomfanya mbunge wa zamani, Venance Mwamoto kuibuka mshindi.
Katika matokeo ya awali kwenye baadhi ya vituo, Profesa Msola aliongoza kwa kura nyingi zaidi ambapo yaliibuka madai ya udanganyifu.
Pia yaliibuka madai ya kuwapo wapigakura wasio na kadi za CCM waliosafirishwa kwenda kupiga kura na mmoja wa wagombea wa ubunge katika Tawi la Kipaduka.
Katika Jimbo la Makete, yaliibuka madai ya dosari kadhaa hali iliyomfanya Katibu wa CCM Mkoa wa Njombe, Hosea Mpagike, kusema kuwa changamoto za miundombinu katika jimbo hilo zimesababisha kuchelewa kwa matokeo.
Katika uchaguzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge alipata kura 8,534 huku mpinzani wake wa karibu, Profesa Norman Sigala akipata kura 8,211, Bonic Muhami 500, Fabianus Mkingwa 466 na Lufunyo Rafael 226.
Hata hivyo, Profesa Sigala alipinga matokeo hayo kwa kuwasilisha malalamiko yake kwa vikao vya juu ambavyo jana vimetoa uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Awali katika Jimbo la Ukonga, matokeo yalikuwa yakimpa ushindi kada wa chama hicho, Ramesh Patel aliyepata kura zaidi ya 10,000 lakini baada ya muda hali hiyo ilibadilika ambapo aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alitangazwa mshindi kwa kura 10,000 huku Patel akipata kura 7,576 hali ambayo ilisababisha mvutano mkali.
Katika Jimbo la Rufiji, awali matokeo yalionyesha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, anayemaliza muda wake, Dk. Seif Rashid alikuwa ameangushwa na mpinzani wake Mohamed Mchengerwa kwa tofauti ya kura zaidi ya 400.
JK NA KIKAO CHA CC
Awali asubuhi ya jana Rais Jakaya Kikwete alifungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM na kuwataka wajumbe kufanya kazi ya kupitia uteuzi wa wagombea ubunge kwa umakini.
Alisema ni vyema kazi hiyo ikafanyika kwa umakini kwani wanachama wanasubiri kujua nani ni nani baada ya kikao hicho.
“Ndugu wajumbe tufanye kazi iliyotukuka kwa siku hizi mbili kwani wanachama wanasubiri kujua nani ni nani na kisha ibakie iyena iyena tu,’’ alisema Kikwete.
Baada ya Kamati Kuu kumaliza kikao hicho, majina yote ya walioteuliwa yatawasilishwa leo katika kikao cha NEC, kwa ajili ya uteuzi wa mwisho.
Awali akitoa taarifa ya akidi ya wanachama, Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, alisema wajumbe waliotakiwa katika kikao hicho ni 32.
Kinana alisema waliopo hadi jana asubuhi ni 25, hivyo akidi hiyo inatosha kwa ajili ya kikao hicho cha Kamati Kuu.
Kikao hicho cha Kamati Kuu ni mwendelezo wa vikao vya chama hicho ambavyo vilianza Jumamosi iliyopita kwa kikao cha sekretarieti.
Juzi jioni kikao cha maadili kilifanyika hadi saa 7 usiku ambapo kilikuwa kikipitia taarifa mbalimbali za wagombea wa chama hicho wanaomba kuteuliwa kuwania ubunge.
SOURCE:Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni