Ukuaji wa uchumi nchini washuka kwa asilimia 2.1....

Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa la Takwimu (NBS), Morrice Oyuke 


Dar es Salaam. Kasi ya ukuaji wa uchumi nchini imeshuka kwa asilimia 2.1 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na kushuka kwa uzalishaji katika sekta za madini, mazao ya chakula, habari na mawasiliano.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa uchumi utaendelea kushuka zaidi kutokana na athari za Uchaguzi Mkuu na mpango wa Serikali wa kubana matumizi yake.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa la Takwimu (NBS), Morrice Oyuke alisema jana kuwa kasi ya Ukuaji wa Pato la Taifa (GDP), imeshuka kutoka asilimia 8.6 2014 hadi kufikia asilimia 6.5 katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema sekta ya madini imefanya vibaya zaidi kutokana na rekodi ya kukua kwa kasi ya asilimia 0.6 katika kipindi hicho, ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 19.7 mwaka 2014.
“Sekta ya madini haijafanya vizuri kutokana na kushuka kwa bei ya madini katika soko la dunia, lakini uzalishaji katika baadhi ya migodi kama Tulawaka umepungua,” alisema.
Oyuke alisema ukuaji wa sekta za kilimo na mifugo umeshuka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2014 hadi asilimia 2.6 kutokana na ukame katika maeneo mengi nchini na kuathiri uzalishaji wa mazao.
Hata hivyo, alisema ukuaji wa uchumi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mafanikio makubwa ya uzalishaji wa nishati ya umeme na maji uliokuwa kwa asilimia 0.6.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Repoa, Profesa Samuel Wangwe alisema kasi ya ukuaji wa uchumi itaendelea kushuka kutokana na Serikali kuminya matumizi katika taasisi zake ambazo huwa ndiyo chachu ya kuukuza.
“Pia, mwaka wa uchaguzi kasi ya uwekezaji huwa inapungua kutokana na tabia ya wawekezaji kusubiri matokeo, hivyo ili uchumi uimarike itachukua takriban miezi sita baada ya Uchaguzi Mkuu,” alisema Profesa Wangwe.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi alisema pamoja na uchaguzi kuathiri ukuaji wa uchumi, bado utachochea kukua kwa baadhi ya sekta za uchukuzi, malazi, huduma za uchapaji, vifaa vya maofisini, chakula na mawasiliano.

SOURCE:Mwananchi











Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..