JK: Dk Magufuli ameniokoa ugomvi na wakwe zangu...

Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kufungua
Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kufungua rasmi Barabara ya Ndundu-Somanga yenye urefu wa kilomita 60, akiwa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli (kulia) na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jassem Ibrahim Al Najem (kushoto) kwenye hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Marendego, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Picha na Ikulu. 

Rufiji. Rais Jakaya Kikwete amesema sasa atazungumza lugha moja na wakwe zake baada ya kukamilika Barabara ya Ndundu-Somanga kwa kiwango cha lami.
Rais Kikwete alisema hayo juzi jioni kwenye sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo iliyofanyika Kijiji cha Marendego Mpakani na kuhudhuriwa na wananchi wa mikoa ya Lindi, Pwani pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali akiwamo Balozi wa Kuwait nchini, Jassem Ibrahim AL- Najem.
“Nimekuwa mwenye furaha sana maana barabara hii ilikuwa ikininyima usingizi kwa sababu mbili; kwanza kuchelewa kumalizika na vilevile kile kilio cha kuhitaji hii barabara ilikua ni kilio cha muda mrefu sana cha wananchi wa mikoa hii ya kusini cha wabunge wao na viongozi wao.
“Lakini siyo hilo pekee, kwa sisi tuliooa mikoa ya huku, imenipa tabu pia, kila wakati naulizwa mbona humalizi barabara ya kwetu, ninasema itaisha, kwa hiyo nafurahi leo ndugu Magufuli (John) umeniondolea unyonge, ninasimama hapa kwa kujiamini. Wakwe zangu na shemeji zangu ugomvi sasa umeisha, kwa hiyo nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitakushukuru Waziri Magufuli. kwa kuwa mstari mbele kusimamia ujenzi huu na hata katika maeneo mengine umekuwa mtendaji wa kuigwa,” alisema Kikwete
Akitoa taarifa ya barabara hiyo Dk Magufuli alisema sehemu hiyo ya kilomita 60 ndiyo iliyokua sehemu pekee iliyobaki kujengwa kwa kiwango cha lami, mradi huo umegharimu Sh77.2bil na kutekelezwa kwa kugharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 55, Mfuko wa Kuwait kwa asilimia 31 na mfuko wa OPEC kwa asilimia 14.
Naye Balozi AL-Najem alisema kwamba ziara ya Rais Kiwete nchini humo ndiyo chimbuko ya mafanikio ya barabara hiyo.
Mapema mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo akitoa salamu za mkoa alisema awali usafiri wa wananchi kutoka Ndundu ilichukua siku mbili hadi tatu kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara au kutoka kwenye mikoa hiyo kuja Pwani na Dar esaaam kutokana na eneo hilo kuwa mbaya na hivyo magari mengi yalikuwa yanakwama kuendelea na safari yakifika hapo lakini sasa safari ni kwa saa,” alisema.
SOURCE:Mwananchi





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..