Rais wa Zanzibar, Dk Shein awaongoza mamia kumzika Prof Ishau
Mwili wa Marehemu Profesa Ishau
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein leo, Jumatano ameungana na mamia ya wananchi katika mazishi ya aliyewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Afisa Mwandamizi (Mstaafu) wa Idara ya Organaizesheni CCM Zanzibar , Prof. Ishau Abdullah Khamis huko kijijini kwao Donge Wilaya ya Kaskazini "B" Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Marehemu Prof. Ishau amefariki juzi, Jumatatu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuuguwa kwa muda mrefu maradhi ya figo.
Katika mazishi hayo Dkt. Shein ameambatana na viongozi mbali mbali wa chama na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi” , Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Vuai Mwinyi Mohamed, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali, Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.
Prof.Ishau amepata elimu yake ya msingi katika Shule ya msingi Donge na kusoma elimu ya Chuo Kikuu Makerere Uganda na baadae kwenda nchini Hungry alikopata kiwango cha elimu ya Uprofesa na kurudi nchini kwa ajili ya kufanya kazi za umma.
Marehemu Prof. Ishau enzi za uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Ubunge, Mwalimu katika Chuo cha Uchumi (Dar), Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi na Waziri wa Utalii na Misitu.
Hadi mauti yanamkuta Prof.Ishau alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Takwimu Zanzibar nafasi ambayo ameteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Source:Azam Tv
Maoni
Chapisha Maoni