Utendaji wa Rais Magufuli wazidi kuwakosha Watanzania..

Rais Magufuli siku alipokula kiapo rasmi kuwa Rais wa Tanzania.



Asilimia 71 ya wananchi wa Tanzania wanaukubali utendaji wa Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza kupitia programu yake ya Sauti za Wananchi mwezi Aprili mwaka huu, kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 96 ya mwezi Juni 2016. 
Akiwasilisha matokeo hayo, Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, amesema kuwa kiwango hicho bado kiko juu ya wastani wa viwango vya kukubalika kwa marais wa Afrika, ambapo wastani wao kama ilivyorekodiwa katika tafiti 128 za utafiti wa Afrobarometer tangu mwaka 1999 ni asilimia 63.
Eyakuze amesema utafiti huo umebaini kuwa Rais Magufuli anakubalika zaidi miongoni mwa vikundi vya wazee na wenye elimu isiyozidi ya msingi.
Pia kiwango cha kukubalika ni kikubwa miongoni mwa wananchi masikini (asilimia 75) kuliko matajiri (asilimia 66) na hakuna tofauti kubwa kati ka viwango vya kukubalika kwa Rais kati ya wanawake (asilimia 73) na wanaume (asilimia 70), au kati ya wakazi wa vijijini (asilimia 72) na mjini (asilimia 70).
Kuhusu hali ya vyama vya siasa, utafiti huo umebainisha kuwa asilimia 63 ya wananchi wanasema wapo karibu zaidi na CCM kuliko chama kingine chochote, huku CHADEMA wakiwa asilimia 17,  CUF asilimi 1, ACT Wazalendo asilimia 1, NCCR asilimia 1 na wasio karibu na chama chochote wakiongezeka kutoka asilimia 4 mwaka 2012 hadi asilimia 17 mwaka 2017.
Viwango hivyo vya kukubalika kwa vyama vinamaanisha kwamba kukubalika kwa CHADEMA kumeporomoka kutoka asilimia 32 ya mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 17 mwaka huu na CUF kikishuka kutoka asilimia 4 mwaka 2013 hadi asilimia 1 mwaka huu huku CCM kikishuka kutoka asilimia 65 ya mwaka 2012 hadi asilimia 62 ya mwaka 2015 na kupanda tena mwaka huu hadi asilimia 63.
Pia utafiti huo umebaini kuwa CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee, wenye kiwango cha chini cha elimu, masikini, wanawake na wakazi wa vijijini huku kinyume chake ikiwa ni aina ya watu wanaokikubali zaidi CHADEMA na kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 84 ya wananchi wamesema watapiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kuhusu kero mbalimbali zinazowakabili wananchi, idadi ya waliotaja upungufu wa chakula kama tatizo kubwa imeongezeka huku waliotaja rushwa ikipungua.
Katika utafiti huo ambao hufanyika kwa njia ya simu, kero kubwa tatu zilizotajwa na wananchi ni pamoja na umasikini (asilimia 60), upungufu wa chakula (asilimia 57) na afya (asilimia 40).

Source:Azamtv

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..