Serikali yatangaza neema kila kona bajeti mpya
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango
Serikali leo,Juni 7 imewasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, huku ikitangaza unafuu kwa kufuta ama kupunguza tozo, ushuru na kodi ya ongezeko la thamani katika sekta mbalimbali .
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amependekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mtaji ili kupunguza gharama za mashine na mitambo kwa ajili uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati, kufuta VAT kwenye bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi kuifanya Tanzania iwe njia bora ya kupitisha bidhaa ili kuongeza mapato kupitia bandari na kusamehe VAT kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa nchini ili kuwapunguzia wafugaji gharama ya vyakula hivyo.
Neema nyingne zilizopendekezwa na Waziri Mpango ni pamoja na Kupunguza kodi za kampuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 kwa miaka mitatu ya uzalishaji, kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari iliyokuwa inalipwa kila mwaka hata kwa magari yasiyotumika, kupunguza ushuru wa mazao kutoka 5% hadi 3% kwa mazao ya biashara na 2% kwa mazao ya chakula na kufuta kabisa ushuru kwa mazao yasiyozidi tani moja yanayosafirishwa kutoka halmashauri moja kwenda nyingine.
Mbali na hizo, Wazir Mpango pia amependekeza kutoza ushuru wa forodha kwa 0% badala ya 25% kwenye malighafi kwa ajili ya vifaa vya watu wenye ulemavu, na kufuta ushuru wa huduma kwenye nyumba za kulala wageni 'Guest House'
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amependekeza kuondolewa kwa ushuru wa huduma unaotozwa na halmashauri kwenye mabango na vibao vya matangazo vinavyoelekeza mahali zilipo huduma muhimu za kijamii kama vile shule na hospitali huku akitangaza rasmi kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu, Mamlaka ya Mapato (TRA) ndiyo watakaokuwa wakihusika na ukusanyaji wa ushuru wa mabango katika halmashauri zote nchini.
Kuhusu vyanzo vipya vya mapato, Dkt. Mpango ametangaza rasmi ukusanyaji wa kodi ya majengo katika miji na vijiji vyote nchini ambapo amesema majengo/nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini kodi yake itakuwa Shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida na 50,000 kwa nyumba za ghorofa.
Akizungumzia deni la taifa, Dkt Mpango amesema deni hilo limeongezeka kwa asilimia 9, kutoka bilioni 39.274 Machi 2016 hadi bilioni 42,883 Machi 2017 na kuwaondoa hofu watanzania kwamba Tanzania bado ina nafasi ya kuendelea kukopa kwa ajili ya miradi yake ya maendeleo.
Kama hatua ya kudhibiti rasilimali za nchi, amesema serikali imepiga marufuku usafirishaji wa madini moja kwa moja kutoka migodini kwa ajili ya kupelekwa nje ya nchi.
Source:AzamTv
Maoni
Chapisha Maoni