Shein kuongoza sala ya Eid kesho..
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kesho, Jumatatu anatarajiwa kuwaongoza waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya sala maalumu ya kusherehekea Sikukuu ya Eid el Fitri.
Msimamizi wa sherehe za Eid, Sheikh Abdallah Talib amesema kuwa mbali ya Dk Shein kuhudhuria ibada ya sala, pia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Eid litakalofanyika katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi la zamani, Mnazi Mmoja mjini hapa.
Talib amesema matayarisho kwa ajili ya ibada zote mbili yamekamilika.
Amesema Ibada ya sala itaanza saa 1.25 asubuhi katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kufuatiwa na Baraza la Eid saa 4.00 asubuhi.
Talib amesema kwa upande wa kamati ya sherehe hiyo, wamejipanga vyema ili kuona shughuli nzima inafanyika katika hali ya amani na utulivu kwa kipindi chote.
“Tumejipanga vizuri katika kufanikisha shughuli hii ili ifanyike katika kiwango kizuri, tayari kila kitu kimekamilika ikiwemo kupanga utaratibu wa kufika wageni wetu waalikwa na mambo mengine yanayohusiana na shughuli hiyo,”amesema.
Alisema kuwa ni wajibu wa kila Muislamu kujitokeza kwa wingi katika ibada hizo ambazo hufanyika kila baada ya kukamilika kwa ibada ya funga ya mwezi wa Ramadhan.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema wamejipanga vyema katika ulinzi na usalama kwa kipindi chote cha kusherekea sikukuu hiyo kwa kuweka ulinzi kila kona.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali amesema jeshi limejipanga vyema ili kuona hali ya amani na utulivu inadumu ndani ya kipindi chote cha sherehe hiyo.
Source:Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni