Wabunge kuingia darasani somo la maadili
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinatarajia kufundisha programu ya uongozi maadilina utawala bora kwa Wabunge ambapo watasoma kwa awamu, mara baada ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti.
Hayo yamesemwa leo (Juni 30) na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Chuo hicho, Evelyne Mpasha jijini Dar es Salaam katika maonesho ya saba saba ya 41 yanayoendelea Jijini humo.
Mpasha amesema, Chuo hicho kilianzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 kikiwa na lengo la kufundisha viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) maadili na uzalendo kwa nchi.
"Tangu kuanza mfumo wa vyama vingi nchini, Chuo kimekuwa kikijihusisha na utoaji wa programu za kitaaluma na kuanzia mwaka 2015 chuo kimerejesha tena kozi ya uongozi na maadili," amesema Mpasha.
Amesema kuwa, kozi hiyo hutolewa kwa viongozi walio katika ngazi ya maamuzi kutoka Taasisi za Umma na Binafsi ambapo hufundishwa masuala ya uzalendo, utaifa na maendeleo ya nchi.
Pia amesema Chuo kimepokea viongozi mbalimbali kutoka katika Halmashauri mbalimbali, Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali kwa ajili ya kujifunza programu hiyo.
Mhadhiri wa Chuo hicho, Tiberius Mlowosa amesema kumekuwepo na viongozi wengi wanao hujumu uchumi wa nchi kutokana na kukosa mafunzo ya uongozi na maadili.
"Kama viongozi wote walio ngazi ya maamuzi wangepata mafunzo ya uongozi maadili na utawala bora, tusingekuwa na masuala ya EPA wala ESCROW," amesema Mlowosa.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinatoa programu nyingine nje ya programu hiyo ya uongozi ambazo ni Utawala na Rasilimali Watu, Usimamizi wa Biashara, Maendeleo ya Jamii, Uhasibu, Ununuzi na Ugavi kuanzia ngazi ya cheti.
Source:Mwnanchi
Maoni
Chapisha Maoni