Waziri mkuu awaasa wazazi katika malezi..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema wazazi wana jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu ili Taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi.
“Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na Taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema.
Alitoa kauli hiyo jana , Jumamosi, Juni 17 wakati akizungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Peter Pinda.
Waziri Mkuu alisema wazazi wanapaswa kujitathmini juu ya malezi ya watoto wao na kujihoji kama wamepata malezi yanayostahili. “Kupitia funzo tulilolipata leo, tujitathmini kuhusu makuzi ya watoto wetu. Je watoto wetu wanapata malezi stahiki? Je tunawalea katika misingi ya kutoa kwa ajili ya Mungu au tunawafundisha wajilimbikizie mali? Je, tunawahoji watoto wetu kuhusu utajiri wanaoupata ghafla? Au tunawapongeza na kufurahia bila kujua wanapata wapi utajiri huo?,” alihoji.
“Nitumie nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya Taifa tunalotaka kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisisitiza.
Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mkewe walichangia shilingi milioni 10 ambapo jumla ya shilingi milioni 160 zilikusanywa. Kati ya hizo, shilingi milioni 11 zilikuwa ni ahadi, na shilingi 10,403,000 zilikuwa ni vifaa vya ujenzi.
Source:Azamtv
Maoni
Chapisha Maoni