Arusha yapokea 1.28 bilioni za elimu bure,yapiga marufuku michango..
Mkoa wa Arusha, umepiga marufuku michango katika shule za msingi na Sekondari ambayo haijaidhinishwa na mkuu wa mkoa huo, baada ya kupokea kiasi cha sh 1.28 bilioni za kugharamia uendeshaji wa shule za Serikali mkoani Arusha.
Akizungumza na mwananchi, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Addoh Mapunda alisema,kuanzia sasa ni lazima michango yote katika shule ipate baraka za bodi za shule na kuidhinishwa na Mkuu wa mkoa Felix Ntibenda.
"Hatutegemei michango isiyo na tija baada ya shule zote kupatiwa fedha za kugharamia uendeshaji"alisema.
Alisema fedha zilizotolewa na Serikali ni kwa ajili ya ada kiasi cha Sh20,000 kwa shule za kutwa na Sh70,000 kwa shule za bweni sambamba na fedha nyingine za uendeshaji katika shule za serikali.
Alisema fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi na Sekondari na akaonya walimu ambao wanatumia fedha hizo kinyume cha taratibu.
Hata hivyo,alisema kumekuwepo na changamoto ya fedha za chakula mashuleni, ambapo sasa wazazi ambao watapenda watoto kula mashuleni,watashirikiana na kamati za shule na baadaye mkuu wa mkoa ili kuwezesha michango.
Maoni
Chapisha Maoni