Zitto akerwa wauguzi vijijini kusahaulika..
Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Zitto Kabwe.
Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Zitto Kabwe amesema watumishi wengi wakiwamo wauguzi wanaofanya kazi vijijini hawapandishwi madaraja licha ya kutoa huduma kwa wananchi.
Alibainisha hayo jana katika ziara ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kubaini changamoto katika huduma za afya wilayani Bariadi na Busega.
Katika ziara hiyo iliyoshirikisha Taasisi ya Benjamin Mkapa, Zito alisema changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya afya ni kuacha kuwapandisha madaraja watumishi, ukosefu wa majengo na madawati.
Pia, alisema changamoto nyingine ni vituo vya afya vijijini kukosa dawa.
Alisema baadhi ya watoa huduma hasa wauguzi wengi wanafanya kazi za uganga katika vituo vya afya kutokana na kutokuwapo kwa wataalamu.
“Tumepita katika sehemu nyingi na kuona changamoto za afya katika vituo vya kutolea huduma hiyo, kubwa kabisa ni ukosefu wa dawa na madaktari, hali inayosababisha hata wahudumu kufanya kazi za udaktari na mshahara wake unabaki palepale bila kupandishwa daraja,” alisema Zitto.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mkapa, Manka Kway alisema lengo la ziara hiyo ni kutatua changamoto za uhaba wa watumishi na uhitaji wa motisha kwa watumishi wa afya hasa wanaofanya kazi katika mazingira magumu.
Kway alisema dhamira ni kuwawezesha wajumbe wa kamati hiyo kuelewa mikakati inayotumiwa na halmashauri za wilaya kutoa motisha ili watumishi waendelee kuisha katika mazingira magumu.
“Taasisi imeona kuwa ipo haja ya kujifunza mbinu mbalimbali zinazotumiwa na halmashauri kuweka mipango endelevu na bajeti madhubuti itakayokidhi haja za kutoa motisha kwa watumishi wa afya kwa lengo la kuwavutia wengine kubaki katika maeneo yao ya kazi vijiji,” alisema.
Pia, taasisi hiyo inasomesha wanafunzi 1,000 katika vyuo mbalimbali nchini na kuajiri watoa huduma 1,100 na kusambazwa vituo vya afya nchini.
Maoni
Chapisha Maoni