Bunge lamsafirisha Bulaya Mwanza - Dar chini ya ulinzi..

Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya akifikishwaMbunge wa Bunda, Ester Bulaya akifikishwa katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam na maofisa wa polisi kwa ajili ya kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, jana. Picha na Said Khamis.

Saa 24 baada ya Mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya kukamatwa na polisi kwa kukaidi wito wa kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu madai ya kufanya vurugu bungeni, jana alifikishwa mbele chombo hicho chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Bulaya alikamatwa usiku wa kuamkia jana jijini Mwanza alikokuwa akihudhuria vikao vya juu vya Chadema na kuwekwa mahabusu hadi jana mchana aliposafirishwa chini ya ulinzi kwa ndege hadi Dar es Salaam.
Aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa saba mchana na alipitishwa katika eneo la watu mashuhuri akisindikizwa na maofisa wawili wa polisi kisha kupakiwa kwenye gari aina ya Landcruiser likisindikizwa na Defender ya polisi hadi ofisi ndogo za Bunge kukutana na kamati hiyo.
Baada ya mahojiano hayo, mbunge huyo aliyehamia Chadema kutoka CCM siku chache kabla ya uchaguzi mwaka jana, alisema kamati hiyo ilikuwa ya kimahakama hivyo asingeweza kusema lolote, ila akashukuru kwa ulinzi aliopatiwa akisema hajawahi kuupata.
Alisema hakuitikia wito wa Kamati ya Bunge kwa sababu alikuwa anaumwa na aliona afya yake ni muhimu kuliko chochote. Baada ya mahojiano hayo alielekea uwanja wa ndege kurudi Mwanza.
Vurugu hizo zilitokea Januari 27 katika mkutano wa 11 wa Bunge baada ya wabunge wa upinzani kupinga uamuzi wa Serikali kusimamisha urushaji wa vipindi vya Bunge moja kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Sakata hilo lilisababisha polisi zaidi ya 50, Usalama wa Taifa na askari kanzu kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kuwatoa wabunge wa upinzani kwa kuwabeba baada ya kukataa amri ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ya kuwataka watoke kwa hiari.
Chenge aliwataja baadhi ya wabunge wa upinzani na kuwataka waende nje kwa madai kuwa walikuwa wanafanya fujo, jambo lililosababisha wenzao wote kusimama na kupinga amri hiyo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo kwa niaba ya Katibu wa Bunge, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya alisema wabunge walioitwa na kamati hiyo ni wanne lakini Bulaya pekee hakutokea.
Alisema baada ya vurugu hizo, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliagiza; Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Bulaya kuhojiwa na kamati hiyo.
“Kamati ndiyo itaamua nini cha kufanya. Kwanza itamhoji na ikumbukwe kuwa kamati inapokuwa inatekeleza majukumu yake inakuwa kama chombo cha Mahakama, hivyo kinaweza kupeleka suala hili kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali ili hatua stahiki zifuate,” alisema Mwandumbya.
Alisema Bulaya alipewa wito huo Machi Mosi na kuusaini akitakiwa kufika kuhojiwa Machi 9 na kwamba siku hiyo kamati ilikaa mpaka saa 11 jioni ikimsubiri lakini hakutokea.
“Kutokana na uamuzi wake wa kutofika, Spika wa Bunge alitumia kifungu namba 15 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ya mwaka 2002 kutoa hati ya kukamatwa na kufikishwa kwenye kamati, agizo ambalo hutekelezwa na polisi,” alisema. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema: “Jeshi la polisi halina madai yoyote dhidi ya mbunge huyo.”





Source:Mwananchi

















































































































































































      

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..