Lukuvi azindua mpango wa kurasimisha makazi..
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, William Lukuvi amezindua mpango wa kitaifa wa kurasimisha makazi ili wamiliki wake waweze kutambuliwa na kupatiwa huduma za kijamii.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, William Lukuvi amezindua mpango wa kitaifa wa kurasimisha makazi ili wamiliki wake waweze kutambuliwa na kupatiwa huduma za kijamii.
Mpango huo umeanzia katika Kata ya Kimara jijini hapa na mitaa iliyoguswa ni Mavurunza, Kilungule A, Kilungule ‘B’, Golani, Kimara Baruti na Baruti.
Lukuvi alisema mpango huo utawasaidia wakazi waliojenga bila kufuata taratibu za mipango miji kutambulika na maeneo yao kuwa na thamani.
Alisema lengo la Serikali kuondoa makazi holela na kuwa halali, hasa maeneo ya pembezoni ni ili haki sawa iwapo katika huduma za zahanati, shule, barabara na masoko.
Pia, waziri huyo aliwaonya vigogo wenye nia ya kuingilia mpango wa kurasimisha makazi holela kwa lengo la kuwadhulumu viwanja wakazi wa maeneo husika kuwa, watachukuliwa hatua za kisheria.
Lukuvi alitoa siku 90 kwa mkuu wa idara ya urasimishaji ardhi ya wizara hiyo kukamilisha mpango wa kupima maeneo hayo na hati za umiliki wa viwanja vikamilike ndani ya mwezi mmoja.
“Nisisikie kuna mwanasiasa ambaye hakuwa anaishi hapa kesho na keshokutwa anakuja kutaka eneo hapa, kwani tunajua wazi kuwa maeneo haya yana wenyewe na mkimuona mtu asiyehusika toeni taarifa,” alisema Lukuvi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango Miji na Vijijini, Immaculata Senje alisema eneo la Chasimba lina hekta 224 na wakazi 4,000 na kwamba, limetangazwa rasmi kuwa la makazi badala ya viwanda.
Senje alisema kutakuwa na akaunti itakayofunguliwa kwa makubaliano kati ya Serikali na Kiwanda cha Saruji Wazo ambayo itatumika kukusanya tozo mbalimbali ikiwa pamoja na ile ambayo itatumika kulipa fidia.
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea alisema mpango huo ukikamilika utasaidia kupeleka huduma za jamii ikiwamo hospitali, masoko na shule.
Maoni
Chapisha Maoni