Precision Air yatamani kuungana na ATCL..


Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la PrecisionAir, Sauda Rajab amesema anatamani kuunganisha nguvu ya shirika lake na Shirika la Ndege Tanzania ili kuona Tanzania inakuwa na ndege zake, huku ikipiga hatua katika nyanja ya usafiri wa anga.
Akizungumza katika mahojiano mafupi hivi karibuni, Sauda alisema kuwa anatamani siku zote kuona kuwa Tanzania inakuwa na shirika lake la ndege na ikiwezekana kuungana na shirika lake.
Alisema kuwa Tanzania ni Taifa linaloheshimika, hivyo ni wakati sasa wa kuwa na shirika la ndege lililosimama imara tofauti na sasa kwamba shirika lina ndege moja ambayo wakati mwingine haina uhakika wa kuruka.
“Kenya wana shirika la ndege imara, kwa sasa tuna uwanja wa kimataifa unaojengwa,ni wakati wa kuwa na shirika imara la ndege, na Tanzania inaweza kuwa eneo la wasafiri mbalimbali kuunganisha ndege. Badala ya wasafiri kwenda Kenya au kwingineko, Tanzania inakuwa kituo kwa watu kubadilishia ndege Tanzania, sasa kufanya hivyo kunaweza kuliingizia Taifa fedha za kutosha,” alisema Sauda.
Kwa upande mwingine, alisema kuwa shirika lake liko sawasawa kwani mpaka sasa linamiliki ndege sita zinazofanya kazi na tatu zikiwa katika matengenezo, huku likikabiliana kwa ushindani na mashirika yanayotoa huduma za usafiri wa ndege nchini
Alisema kuwa ili kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika biashara ya ndege, inatakiwa kuimarisha viwanja vyake ili usafiri wa ndege uwe wa uhakika kwa wakati wote kwa mikoa yote, tofauti na sasa, ndege zinatua kwa baadhi ya mikoa.
Sauda alisema kuwa Uwanja wa Ndege wa Songwe ukiimarishwa zaidi ikiwamo kuwekewa taa, utakuwa kiunganishi kizuri kwa wafanyabiashara wa Malawi, Zambia na hata DR Congo sanjari na Tabora ambao unaweza kuwa kiungo cha mkoa huo na mikoa ya Kati na Kanda ya Ziwa.
Alisema shirika kwa sasa limejitanua kwa kiasi kikubwa likiwa na hanga lake huku likiendelea kufanya kazi kibiashara zaidi kwa kutengeneza wataalamu wa kusaidia katika kuongoza ndege zake.
Shirika hilo linazalisha mafundi, waongoza ndege na wadhibiti ubora wa ndege ambao kundi la kwanza la mafundi linatarajia kumaliza mafunzo yake, Septemba mwaka huu.     


Source:Mwananchi
































































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..