RC DAR AMTAKA MEYA WA KINONDONI KUACHA MALUMBANO...
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadki.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amemtaka Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniphace Jacob, kuacha malumbano ya kisiasa na badala yake ajikite kufanya kazi.
Ushauri wa Sadiki umekuja baada ya Meya Jacob kukaririwa akisema manispaa hiyo ina uwezo wa kukabiliana na uamuzi wa serikali wa kutoa elimu ya bure bila kuhitaji fedha zinazotolewa na utawala wa Rais John Magufuli.
Halmashauri ya wilaya ya Kinondoni inaongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao ni mwamvuli unaojumuisha wabunge na madiwani kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).
Sadiki alisema hahitaji malumbano na kiongozi huyo ambayo hayana tija.
“Mimi sipendi malumbano yasiyo na tija baina ya viongozi,” alisema Mkuu wa Mkoa kwa sababu “unapokataa msaada kama huo wa kupunguza mapungufu katika sekta ya elimu, wanaoathirika ni watu waliowachagua.”
Serikali imepanga kutumia Sh. Bilioni 137 kugharamia elimu bure katika miezi sita ya kwanza ya Rais wa tano, Magufuli.
Kiasi cha Sh. bilioni 18.77 kilitumwa kwenye akaunti za shule za Msingi na Sekondari za halmashauri zote hapa nchini na vyombo vya usimamizi wa mitihani kwa kila mwezi wa Januari na Februari, kwa ajili ya wanafunzi kusoma bure.
Source:Mtembezi.com
Maoni
Chapisha Maoni