Dk Mashinji, katibu mkuu Chadema.
Katibu Mkuu mpya wa Chadema Dk Vincent Mashinji. Picha na Michael Jamson
Dk Vincent Mashinji amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chadema akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Willibrod Slaa aliyeachana na chama hicho siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Dk Mashinji ambaye kitaaluma ni daktari binadamu alichaguliwa baada ya jina lake kuwasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa Kamati Kuu ilipokaa chemba na baadaye mbele ya Baraza Kuu na kupitishwa kwa kura za kunyoosha mikono na kuwaacha wajumbe midomo wazi kwa kuwa awali walikuwa wanayazungumza majina mengine yaliyozoeleka.
Dk Mashinji anakuwa katibu mkuu wa nne wa Chadema tangu chama hicho kianzishwe baada ya Bob Makani, Dk Walid Aman Kabourou na Dk Slaa.
Mara baada ya kuchaguliwa, Dk Mashinji aliwataka wanachama wa Chadema washirikiane kujenga mfumo badala ya kuacha jukumu hilo kwa watu wachache.
Dk Mashinji ambaye alishiriki katika kuandaa Ilani ya Uchaguzi ya Chadema na Ukawa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alisema atajifunza na atashaurika.
Akizungumzia uteuzi wake, Dk Mashinji alisema Mbowe alimwalika katika chakula cha mchana (bila kutaja siku) na kumdokeza juu ya kumpa nafasi hiyo. “...sikuamini lakini Mbowe akaendelea kunisisitizia.”
Ni nani?
Dk Mashinji aliyezaliwa katika Wilaya ya Sengerema, alianza elimu ya msingi katika Shule ya Iligamba Januari 1981 hadi Oktoba 1987 na kisha kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Makoko Seminari kuanzia Januari 1988 mpaka Oktoba 1991 alipohitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe kuanzia Julai 1992 hadi Juni 1994 alipohitimu kidato cha sita.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere Uganda mwaka 1995 hadi alipohitimu mwaka 2001 na kutunukiwa shahada ya udaktari. Mwaka 2003 hadi 2005 alisomea Shahada ya Uzamili ya Anaesthesiology katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) na mwaka 2007-2010 alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge ya Sweden ambako alisomea Shahada nyingine ya Uzamili, safari hii katika Utawala na Biashara (MBA).
Hivi sasa ni mwanafunzi wa Shahada nyingine ya Uzamili katika Afya ya Jamii anayosomea Chuo Kikuu cha Roehampton, Uingereza na pia Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria.
Maoni
Chapisha Maoni