Makamu wa Rais Kenya azungumzia tukio la uvamizi nyumbani kwake
Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amezungumzia tukio la watu wenye silaha kuvamia nyumbani kwake jana majira ya mchana na kupambana na vikosi vya usalama.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, watu hao wenye silaha wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Ruto eneo la Sugoi majira ya saa saba mchana na kwamba baada ya kumzidi nguvu mlinzi aliyekuwa getini waliingia ndani na kupambana na vikosi vya ulinzi kwa kwa takribani saa mbili.
Akizungumzia tukio hilo leo katika uwanja wa Ihura, Ruto amesema watu hao walikuwa na lengo la kuvunja umoja na amani iliyojengeka ndani ya nchi hiyo.
“Najua watu wengi mnafahamu kwamba jana nilikuwa na ugeni nyumbani kwangu, watu wema sana… lakini nataka kusema kwamba wanaodhani watavuruga umoja wetu au kuturudisha nyuma hawatafanikiwa,” alisema Ruto.
“Natoa wito kwenu msiharibiwe na aina ya watu ambao wana lengo la kuvuruga maendeleo ya umoja wetu kama taifa,” aliongeza.
Ruto na familia yake hawakuwa nyumbani wakati tukio hilo la uvamizi lilipotokea. Helkopta ya Polisi ilionekana juu ya eneo la nyumba ya Ruto majira ya saa tisa kasoro na vikosi vya usalama viliwadhibiti watu hao.
Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya kuripotiwa tukio la kundi la Al-shabaab kuteka gari lililokuwa kwenye msafara wa kampeni za Jubilee katika eneo la Mandela, mpakani mwa nchi hiyo na Somalia.
Mkuu wa polisi wa kituo cha Mandela South, Charles Chacha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa juhudi za kuwaokoa watu waliokuwa ndani ya gari hilo zinaendelea.
Kenya inajiandaa kupiga kura kwenye uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Source:Dar24
Maoni
Chapisha Maoni