Wizara ya Afya yaanzisha rejesta ya wanaohisiwa kuwa na kifua kikuu..
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeanzisha rejesta ya wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu itakayowekwa katika kila ngazi ya utoaji wa huduma za afya nchini.
Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu amesema hayo katika mkutano wa kupitia utekelezaji wa mkakati wa uboreshaji wa kasi ya uibuaji wa wagonjwa wa kifua kikuu.
katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari (Maelezo), Waziri Mwalimu amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha mkakati huo unatekelezwa kwa ufanisi.
Amesema jana (Julai 4) kuwa, “Tayari rejesta hizi zimesambazwa na kuanza kutumika katika mikoa 16.”
Amesema mkakati wa uboreshaji kasi ya uibuaji wagonjwa wa kifua kikuu umejaa mbinu za uendeshaji ili kuvipa uwezo vituo vya huduma za afya kufanya uchunguzi wa kina kwa kila mteja anayepata huduma vituoni na kuwapata wote wenye kuugua kifua kikuu na kuwaanzishia matibabu.
Amesema mkakati huo unahusisha zana zinazotoa mwanga na kuangaza njia bora za kuchunguza kifua kikuu na kubaini wote wenye kuugua ugonjwa huo mijini na vijijini.
Mkakati huo pia unatoa fursa kwa kila kitengo kujitathmini ili kuweka misingi timilifu ya uchunguzi wa kifua kikuu kwa wote wanaohudhuria matibabu katika eneo husika.
Mwalimu amesema utekelezaji wa mkakati huo ulianza Julai mwaka jana katika vituo vya mikoa ya Mbeya na Dodoma na sasa unatekelezwa kwenye mikoa 16, wilaya 48 na vituo 187 nchini.
Source:Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni