Wabunge wanane CUF wapoteza rasmi ubunge wao...
Spika Job Ndugai
Wabunge Wanane wa Bunge la Tanzania waliosimamishwa uanachama na chama chao cha CUF, wamepoteza rasmi ubunge wao baada ya Spika wa bunge hilo, Job Ndugai kutangaza kuwa nafasi hizo ziko wazi.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatano na ofisi ya bunge imeeleza kuwa Spika Ndugai amejiridhisha kuwa wabunge hao wamefukuzwa uanachama kulingana na taratibu za chama hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na ubunge.
“Kwa mamlaka aliyonayo kwa kuzingatia kifungu cha 67(1)(b) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kikisomwa pamoja na kifungu 37(3) cha Sheria ya Uchaguzi Sura 343 kama ilivyojadiliwa Mwaka 2015, mheshimiwa spika huyo ametangaza nafasi hizo kuwa wazi,” Imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Spika pia amemuandikia mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili aendelee na hatua zinazostahili kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Wabunge waliopoteza ubunge wao kupitia sakata hilo ni pamoja na Severina Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed.
Source:Azamtv
Maoni
Chapisha Maoni