Karatasi za kura kuwasili Jumatatu Kenya...
Muonekano wa baadhi ya karatasi zitakazotumika kwenye uchaguzi mkuu Kenya.
Ndege mbili zilizobeba karatasi za kupigia kura kwa nafasi ya urais ambazo zitatumika kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8 nchini Kenya, zitaanza kuwasili nchini humo kuanzia Jumatatu ya Julai 31, huku nyingine zikitarajiwa kufika Agosti 1.
Meneja mkuu wa kampuni Al Ghurair, iliyopewa mamlaka ya kuchapisha karatasi hizo Lakshmanan Ganapathy, amethibitisha kuwa usiku wa Julai 27, ndiyo siku ya kukamilika kazi hiyo ambayo inafanyikia jijini Dubai.
Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchiuni Kenya (IEBC) Roselyn Akombe, amesema baadhi ya maeneo yenye usalama duni kama vile Lamu, Garissa, Mandera, Tana River na Wajir, karatasi hizo zitapelekwa kwa ndege na si barabara.
“Tume inachukua hatua madhubuti kupunguza makosa na kupotea kwa muda miongoni mwa vitu vya kipekee, ikiwemo fomu za kuhifadhia matokeo kuchapishwa awali zikiwa na taarifa muhimu za wagombea” alisema Akombe
Kamishna mwingine wa IEBC, balozi Paul Kurgat, amesema tume kwa nguvu zote inawashauri wapiga kura wote ambao wana haki ya kutekeleza zoezi hilo, kuchukua karatasi sita za kupigia kura siku ya uchaguzi, ili kuepusha kuwepo kwa idadi ndogo ya kura kwa baadhi ya nafasi ikilinganishwa na nyingine.
Source:Azamtv
Maoni
Chapisha Maoni