CHADEMA YAITAKA SERIKALI KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA KUFUFUA UCHUMI...
Chama cha Chadema kimevunja ukimya kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini, na kudai kuwa hali ni mbaya huku ikiitaka serikali kuandaa mpango mkakati wa haraka wa kufufua uchumi.
Wakati akisoma tamko la Kamati Kuu ya Chadema leo Julai, 31, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, amedai kuwa, tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani uchumi wa taifa umeporomoka kutokana na usimamizi mbovu na maamuzi ya papara katika masuala ya biashara, uwekezaji, uandaaji na utekelezaji wa bajeti.
Mbowe ametaja baadhi ya vigezo vinavyoashiria hali ya uchumi kuwa mbaya ikiwemo kudorola kwa sekta ya kilimo na kupelekea bei ya vyakula hasa vya nafaka kupanda, hali ya ukata katika mzunguko wa fedha, kupungua kwa mikopo ya benki za biashara katika sekta muhimu za kiuchumi, na kuongezeka kwa deni la taifa.
“Kwa ujumla mwendo wa uchumi wetu ni mbaya mauzo ya nje yameporomoka, manunuzi kutoka nje yameporomoka, mikopo sekta binafsi imeporomoka, deni la taifa linapaa kuliko kipindi chote, biashara zinafungwa. Bado serikali inasema uchumi unakua? Ni wito kwa wachumi kufanya uchunguzi wa kina tusiingie kwenye mkumbo wa kupika takwimu za uchumi ili kupata umashuhuri wa kisiasa,” amesema na kuongeza.
“Siku zote tukumbuke mficha ugonjwa kifo humuumbua wananchi sasa wanaumizwa kihakika na hali ngumu ya maisha. Serikali inapaswa kuelewa hili na kuweka haraka mpango mkakati wa muda mfupi wa kurekebisha mserereko huu. Taifa halipaswi kubweteka na matukio ya Makinikia ufisadi wa escrow na mengineyo.”
Aidha, Mbowe amedai kuwa kuongezeka kwa deni la taifa la ndani na la nje ndiyo mzizi wa mdororo wa uchumi, kwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kulipa deni kila mwezi sambamba na kulipa mishahara ya watumishi wa umma ukilinganisha na mapato yanayokusanywa kwa mwezi, kitendo kinachopelekea serikali kushindwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani na kulazimika kukopa mikopo yenye masharti magumu.
“Tatizo la kuongezeka na uhimilivu wa deni la taifa ni hoja iliyoibuliwa na CAG alisema deni linaua taifa hii si ripoti ya kupika ni ya CAG, sheria ya kusimamia deni imepitwa na wakati, kwa muda mrefu tumehitaji bunge kuambiwa serikali inapotaka kukopa. matokeo yake deni linaongezeka kwenye matumizi ya kawaida badala ya maendeleo,” amesema.
Source:Modewjiblog
Maoni
Chapisha Maoni